Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika sekta ya usafiri wa anga, huku takwimu rasmi zikidhihirisha mwelekeo chanya wa ukuaji wa safari za ndege, idadi ya abiria na usafirishaji wa mizigo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo, Februari 26, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 sekta ya anga imeendelea kuimarika kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya viwanja vya ndege unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), idadi ya safari za ndege imeongezeka kutoka safari 148,897 mwaka 2023/2024 hadi safari 149,835 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 0.6.

Aidha, idadi ya abiria imeongezeka kutoka abiria milioni 5.15 mwaka 2023/2024 hadi milioni 5.25 mwaka 2024/2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.0.

Ongezeko hilo linaonesha kuimarika kwa safari za ndani na kimataifa pamoja na kuongezeka kwa imani ya wasafiri katika huduma za anga nchini.

"Katika eneo la usafirishaji wa mizigo, takwimu zinaonesha ukuaji mkubwa zaidi. Kiasi cha tani za mizigo kimeongezeka kutoka tani 34,620 mwaka 2023/2024 hadi tani 37,683 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 8.8." Amesema Msigwa.

Pia ameeleza kuwa ukuaji huo unaashiria kuimarika kwa biashara na shughuli za kiuchumi zinazotegemea usafiri wa anga.

"Mwenendo wa nusu mwaka wa Julai hadi Disemba 2025 nao umeonesha kasi ya juu zaidi ya ukuaji. Katika kipindi hicho, safari za ndege zimeongezeka kutoka 83,647 (Julai–Disemba 2024) hadi 91,760 (Julai–Disemba 2025), sawa na ongezeko la asilimia 10." Amesema

Idadi ya abiria katika kipindi hicho imeongezeka kutoka 2,819,912 hadi 3,071,081, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9, hali inayoonesha mwelekeo thabiti wa kupanuka kwa soko la usafiri wa anga nchini.

Serikali imeeleza kuwa ukuaji huu umechangiwa na maboresho makubwa ya miundombinu katika viwanja vya ndege 61 vinavyosimamiwa na TAA, pamoja na kuimarika kwa mifumo ya usalama na huduma kwa abiria na mizigo.

Kwa ujumla, takwimu hizo zinaonesha kuwa sekta ya usafiri wa anga inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi, ikiimarisha mchango wake katika biashara, uwekezaji na utalii, huku ikiweka msingi imara wa mipango ya maendeleo ya baadaye.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...