Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
SERIKALI imezindua Katalogi ya Kwanza ya Ubunifu ya MAKISATU, jukwaa linalowakutanisha watafiti na wanasayansi ili kuonesha tafiti na bunifu zao ili kuzifikisha kwenye matumizi ya jamii na soko kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Februari 23, 2026 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mihaed Omar, alisema mashindano hayo yamelenga kuwaunganisha watafiti ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi kila mmoja katika eneo lake.
Alisema katalogi hiyo itawezakusaidia kufahamika kwa nani amefanya tafiti gani ili kuwasaidia kupata wadau,washirika, na kusaidia bunifu hizo kufika sokoni.
"hatua hii ni sehemu ya mchango katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kuifikisha nchi katika uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.
Ili kufikia malengo hayo tunahitaji tafiti za kutosha, wabunifu wengi na ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu,"alisema dk Omary.
Aliongeza kuwa maboresho makubwa katika sekta ya elimu ni muhimu, akitaja utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 iliyofanyiwa mapitio.
Kwa mujibu wake, sekta ya kilimo ni miongo mwa sekta za kipaumbele zitakazochochea uchumi kufikia malengo yaliyowekwa, kutokana na uwezo wake wa kuzalisha ajira nyingi na kuchangia pato la Taifa.
Alitolea mfano zao la pamba, akisema kuuza mazao ghafi kunawaweka wakulima katika hatari ya kuyumba kwa soko la dunia, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao kupitia ubunifu ili wakulima wanufaike zaidi na kupata masoko ya uhakika.
Aliwataka wabunifu kuzingatia maandiko mbalimbali ya serikali yaliyobainisha changamoto katika sekta ya kilimo, ikiwemo Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Kilimo, ili bunifu zao ziendane na changamoto zilizopo kama tija ndogo na upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos mos Nungu alisema uzinduzi huo umefungua fursa ya ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali na wabunifu kupitia sekta tofauti za kiuchumi, kwa lengo la kuhakikisha bunifu zinaendelezwa na kufikishwa sokoni.
Alisema kupitia jukwaa hilo, wabunifu watatambulishwa kwa jamii na kupewa fursa ya kuendeleza miradi yao, huku akitoa wito kwa wadau wengine kushirikiana katika kuendeleza tafiti na ubunifu nchini.
Naye, Ronald Tran Ba Huy, Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, alisema “Shirika la Mpango wa Chakula Duniani tunakusanya ubunifu huu wote katika sehemu moja ili kuleta mwonekano, kuhamasisha ushirikiano, na kufungua fursa za uwekezaji, msaada wa sera, pamoja na upanuzi wa suluhisho hizi kwa kiwango kikubwa.”alisema
Aliongeza kuwa: “Tunaamini kwa dhati kwamba maendeleo endelevu yanahitaji suluhisho zinazoongozwa na wadau wa ndani, zikisaidiwa na taasisi imara na kuwezeshwa kupitia ushirikiano thabiti.
“Ndiyo maana ushirikiano wetu na COSTECH, pamoja na Serikali ya Tanzania ni wa muhimu sana. Kwa kuwaleta wabunifu hawa pamoja katika sehemu moja, hatuongezi tu kasi ya mawazo na miradi yao, bali pia tunajenga mfumo shirikishi unaowawezesha kukua, kustawi na kuleta matokeo ya kudumu kwa jamii kote Tanzania,” alisema.
Viongozi hao walitoa wito kwa vijana na watafiti kujitokeza kushiriki katika fursa za ubunifu, wakisema mazingira ya kuendeleza bunifu yanaendelea kuboreshwa ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
mbunifu Elina Maseta mmoja wa wanufaika wa Costech, alisema alipata msaada katika safari yake ya utafiti uliolenga kutatua changamoto ya upungufu wa madini chuma kwa watoto wa shule za msingi.
Alisema alianza na wazo la kutengeneza biskuti zenye virutubisho kwa kutumia malighafi za ndani, akapatiwa msaada wa kitaalamu na kifedha hadi kuanzisha uzalishaji.
“Sasa ninazalisha biskuti, mikate na bidhaa nyingine. Tunatumia malighafi zinazopatikana hapa nchini, hivyo kupunguza gharama na kuwapa soko wazalishaji wa ndani na kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo nchini,"alisema














Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...