Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yoichi Mikami, kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya TEHAMA, Anga za Juu na Maendeleo ya Kidijitali.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Kairuki ameishukuru Japan kwa ushirikiano wa muda mrefu katika maendeleo ya Tanzania, akitaja miradi mikubwa kama miundombinu ya nishati ya Kinyerezi I & II kuwa vielelezo vya uhusiano imara kati ya nchi hizo mbili. Pia amepongeza mafanikio ya ushiriki wa Tanzania katika EXPO 2025 Osaka na Kongamano la Biashara na Uwekezaji la TEHAMA lililofanyika Tokyo mwishoni mwa mwaka 2025.

Waziri Kairuki alieleza kuwa moja ya maeneo ya kimkakati katika ushirikiano wa sasa ni mradi wa KiboCUBE unaotekelezwa kwa kushirikiana na JAXA na Taasisi ya Teknolojia ya Kyushu (KYUTECH), ambao utawezesha Tanzania kuzindua satelaiti yake ya kwanza, TanzaniteSat-1. Alisema mradi huo utafungua ukurasa mpya kwa Tanzania kuingia katika sekta ya anga na matumizi ya Teknolojia ya Satelaiti.

Aidha, alibainisha kuwa kupitia JICA, Tanzania inanufaika na Mradi wa Kuimarisha Mpango wa Kitaifa wa kukuza Kampuni changa sambamba na mpango wa kuanzisha Kituo cha Kisasa cha Ubunifu (Innovation Hub) jijini Dar es Salaam ili kukuza vipaji vya vijana na Maendeleo ya Teknolojia.

Katika eneo la rasilimali watu, Waziri Kairuki aliomba kuongezwa kwa fursa za ufadhili kupitia programu ya Japan Africa Dream Scholarship (JADS), hususan katika masomo ya Uhandisi wa Anga, Uchambuzi wa Data za Satelaiti na Akili Unde (AI), ili kuimarisha utaalamu wa ndani.

Kwa upande wake, Balozi Mikami ameipongeza Serikali kwa juhudi za kujenga uchumi wa kidijitali na kuahidi kuwa Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha ajenda ya mabadiliko ya kidijitali na maendeleo endelevu.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...