Na Belinda Joseph, Arusha

Shirika lisilo la Kiserikali la ECHO East Africa limegawa zaidi ya miche 3,000 kwa wakazi wa kijiji cha Ngaramtoni, mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha upandaji miti kwa lengo la kurejesha rutuba ya ardhi na kukabiliana na changamoto ya ukame.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa miche hiyo iliyofanyika Ngaramtoni ya Juu, Mkurugenzi wa ECHO East Africa, Bw. Charei Munene, amesema kuwa shirika hilo limekuwa likifanya kazi katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa zaidi ya miaka 13, likijikita katika masuala ya mazingira na kilimo endelevu.

Bw. Munene amesema kuwa mwaka huu pekee taasisi hiyo imefanikiwa kugawa zaidi ya miche 30,000 katika maeneo mbalimbali ya Arusha na mikoa mingine ikiwemo Kondoa, ikiwa ni mkakati wa kuimarisha uhifadhi wa mazingira na usalama wa chakula.

“Tunawahimiza wakulima kupanda miche ya malisho, si kutegemea nyasi pekee, bali pia kupanda miti inayoweza kutumika kama chakula cha mifugo. Miti hii husaidia kuongeza upatikanaji wa malisho hata wakati wa kiangazi,” amesema Bw. Monene.

Ameeleza kuwa eneo la kaskazini, likiwemo Ngaramtoni, hukumbwa na vipindi virefu vya ukame vinavyoathiri uzalishaji wa mazao na mifugo, hali inayowalazimu wakulima kuchukua hatua za muda mrefu za kukabiliana na athari hizo.

“Wakulima wengi hawajajiandaa vya kutosha kukabiliana na ukame. Lakini unapopanda miti ya kutosha na kuwa na chakula cha akiba cha mifugo, wanaweza kustahimili hata vipindi vigumu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Afisa wa Kitengo cha Kilimo Endelevu kutoka ECHO East Africa, Bi. Marry Mnyabuta, amesema kuwa wakulima wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mnyororo mdogo wa thamani katika sekta ya kilimo, hali inayochangia kipato kidogo kwa wazalishaji.

Amesema suluhisho la kudumu ni kuimarisha kilimo cha miti na kuunda kamati za kijamii zitakazosimamia upandaji na utunzaji wa miti kwa ufanisi.

“Tunasisitiza umuhimu wa jamii kushiriki moja kwa moja katika kutunza miti wanayoipanda. Kupitia kamati hizi, tunaweza kujenga ustahimilivu wa muda mrefu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Bi. Mnyabuta.

Baadhi ya wakazi wa Ngaramtoni wameeleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema tayari umeanza kuleta manufaa katika shughuli zao za kila siku.

Helena Naftary, mkazi wa kitongoji cha Seuri anayejishughulisha na ufugaji wa ng’ombe, amesema miti waliyoipokea imekuwa msaada mkubwa hasa katika kipindi cha kiangazi.

“Zamani kipindi cha kiangazi kilikuwa kigumu sana kwa sababu majani yalikuwa yanakauka na chakula cha mifugo kupungua. Lakini sasa miti hii inatusaidia kupata majani ya kukatia ng’ombe hata wakati wa ukame kama huu,” amesema.

ECHO East Africa limewataka Watanzania kuendelea kushiriki kikamilifu katika upandaji miti kama njia ya kulinda mazingira, kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...