Na Farida Mangube, Morogoro

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imetakiwa kuimarisha misingi ya nidhamu, uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yake ili iendelee kuwa chachu ya maendeleo ya elimu endelevu nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi, Abdul Maulid, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wakati wa mkutano wa 16 wa Baraza la Wafanyakazi wa TEWW uliofanyika mkoani Morogoro.

Amesema kuwa licha ya changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, watumishi wanapaswa kushirikiana kwa weledi, kuzigeuza changamoto kuwa fursa na kuimarisha ubunifu, hususani katika kukabiliana na changamoto za kifedha.

Aliishauri TEWW kupanua wigo wa utoaji wa programu na kubuni vyanzo mbadala vya mapato kupitia uandishi wa maandiko ya miradi mipya, hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya ndani na kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi, Maulid alitaja Programu ya Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (IPOSA) na Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP-AEP).

Amesema TEWW, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, inatekeleza ujenzi katika halmashauri 30 za mikoa ya Manyara, Shinyanga, Simiyu, Singida, Pwani na Tanga.

Amebainisha kuwa jumla ya karakana 27 zimekamilika na zinawasaidia vijana walio nje ya mfumo rasmi kupata mafunzo ya ufundi, stadi za maisha, ujasiriamali pamoja na stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu. Zaidi ya shilingi bilioni 1.55 zimetumika kukamilisha ujenzi huo.

Katika mradi wa SEQUIP-AEP unaotekelezwa kuanzia mwaka 2022 hadi 2025, jumla ya wasichana 13,272 waliokatiza masomo ya sekondari wamesajiliwa katika vituo 191 vinavyosimamiwa na TEWW. Aidha, mwaka 2025 wavulana 1,731 wamesajiliwa, sawa na asilimia 111 ya lengo lililowekwa.

Amesisitiza kuwa Baraza la Wafanyakazi lina wajibu wa kusimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi yote ya kimkakati ili kuhakikisha matokeo yake yanawanufaisha wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa TEWW, Profesa Philipo Sanga, amesema taasisi imefanikiwa kujenga madarasa na majengo ya utawala katika mikoa 14 na kukarabati majengo katika mikoa 8, hatua inayoonesha matumizi yenye tija ya fedha za Serikali.

Ameongeza kuwa taasisi itaendelea kuendesha vikao vya Baraza kwa mujibu wa matakwa ya kisheria ili kuimarisha ushirikishwaji na utawala bora.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...