IKIWA taarifa na elimu ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto za afya ripoti inaeleza waandishi wa habari za afya wanakumbwa na hali inayofanya wasitekeleze wajibu wao unaosaidia ustawi sekta hiyo barani Afrika.

Hayo yameelezwa kwenye ripoti ya mwelekeo wa Vyombo vya Habari vya Afya Afrika 2026, iliyozinduliwa Leo Februari 26, Feb na FINN Partners.

Pia ripoti hiyo inaangazia mwelekeo mpya unaokua wa uandishi wa habari unaozingatia suluhisho na unaoongozwa na Waafrika, ambao unaweza kubadilisha namna masuala ya afya yanavyoripotiwa barani humo.

Ripoti hiyo inatokana na maoni ya waandishi wa habari, wahariri na watetezi kutoka nchi 11 za Afrika, na inatoa taswira halisi ya jinsi habari za afya zinavyoripotiwa pamoja na mahitaji muhimu ya kuimarisha mchango wa vyombo vya habari katika kuboresha matokeo ya afya ya umma.

Waandishi wa habari za afya kwa sasa wanakabiliana na changamoto kadhaa, ikiwemo kupungua kwa ufadhili wa wafadhili, kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari na matatizo ya afya ya akili, milipuko ya mara kwa mara ya magonjwa ya kuambukiza, pamoja na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya. Wakati huo huo, vyumba vya habari vinafanya kazi kwa rasilimali chache, kupungua kwa madawati maalum ya afya, na upatikanaji mdogo wa takwimu sahihi na za wakati.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Peter FINN, Mwanzilishi Mshirika na Mtendaji Mkuu wa FINN Partners amesema kuwa uandishi wa habari za afya ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha hali ya afya za Waafrika.

“Tuko katika wakati muhimu sana kwa mawasiliano ya afya barani Afrika. Uandishi wa habari unapokosa rasilimali za kutosha, afya ya umma huathirika. Mifumo imara ya afya inahitaji mifumo imara ya vyombo vya habari, na hiyo inamaanisha kuwachukulia waandishi wa habari kama washirika muhimu, si wasambazaji wa taarifa tu.”

Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa mabadiliko katika ufadhili wa afya duniani yamekuwa mada kuu katika vyombo vya habari, yakizisukuma nchi kufikiria upya uhuru wa sekta ya afya, ufadhili wa ndani na uzalishaji wa ndani. Wakati huo huo, waandishi wa habari wanajitahidi kutafsiri mabadiliko hayo ya sera na kuyaonesha kwa namna yanavyoathiri maisha halisi ya wananchi.

“Namna masuala ya afya yanavyoripotiwa huathiri imani ya umma, vipaumbele vya sera na hatimaye uimara wa mifumo ya afya,” alisema Maryam Bigdeli, Mtaalamu wa Mifumo ya Afya na aliyewahi kuwa Mwakilishi wa World Health Organization nchini Morocco.

Maryam aliongeza kuwa “Katika kipindi hiki cha mabadiliko ya vipaumbele vya afya duniani na vikwazo vya ufadhili, nchi za Afrika zinapaswa kujikita katika kujenga mifumo imara inayotegemea huduma bora za afya ya msingi, ufadhili endelevu na utawala unaowajibika. Ripoti hii inaonesha umuhimu wa suluhisho za ndani na mjadala unaotegemea ushahidi ili kuhakikisha usawa na uimara wa mifumo ya afya kwa muda mrefu.”

Licha ya changamoto hizo, ripoti imebaini mwelekeo chanya ambapo waandishi wa habari wanazidi kuzingatia uandishi unaotumia takwimu na unaolenga suluhisho, huku ukitoa nafasi kubwa kwa wataalamu na muktadha wa Kiafrika. Waandishi wa habari wanatoa wito kwa wataalamu, watafiti na watendaji wa Kiafrika kunukuliwa zaidi kama vyanzo vikuu vya taarifa, na hivyo kubadilisha taswira ya Afrika kutoka kuwa mhanga wa matatizo hadi kuwa sehemu ya suluhisho.

“Matokeo ya ripoti hii yanaakisi hali halisi tuliyonayo,” alisema Sheriff Bojang, mwandishi wa The Africa Report. “Waandishi wa habari wana hamu kubwa ya kusimulia hadithi zenye athari, lakini wanakabiliwa na ukosefu wa rasilimali na upatikanaji mdogo wa wataalamu wa ndani wanaoaminika. Sasa tunahama kutoka kunukuu tafiti za Magharibi pekee na kuelekea katika kuwasilisha habari za afya kwa muktadha wa ndani. Ripoti hii inatoa mwongozo muhimu kwa mashirika ya afya kusaidia vyombo vya habari ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi.”

Ripoti hiyo inahitimisha kwa kutoa wito kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, wafadhili na sekta binafsi kuwekeza katika uandishi wa habari wa ndani, kuboresha upatikanaji wa takwimu na wataalamu wa Kiafrika, pamoja na kujenga ushirikiano wa muda mrefu unaojengwa juu ya uaminifu ili kuimarisha afya ya umma barani Afrika.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...