Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema ushirikiano wa Tanzania Bara na Zanzibar ni nguzo muhimu katika kukabiliana na athari za mazingira.
Amesema hayo wakati wa kikao cha ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kilichofanyika leo Februari 17, 2026, Zanzibar.
Katika kikao hicho ngazi ya Mawaziri, Dkt. Dugange ambaye ni Mwenyekiti Mwenza alihimiza ushirikiano madhubuti baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika utekelezaji wa shughuli za kimazingira ambao utasaidia katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira.
Alisema suala la mazingira halina mipaka linaihusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hata kama changamoto zinatokea nje ya mipaka ya taifa bado SJMT na SMZ zinashirikiana kwa karibu katika kuweka mazingira vizuri.
“Lazima tushikamane mara kwa mara kuhusu masuala ya biashara ya kaboni mazingira, chochote cha Bara na Zanzibar lazima tuongee lugha moja, hatuwezi kufanya vizuri sana kama hatushirikiani, hivyo niwapongeze Makatibu Wakuu kwa kuona umuhimu wa kukutana na kujadili masuala ya mazingira na kufikia malengo,” alisisitiza.
Hivyo, Naibu Waziri alitoa rai kwa wajumbe wa kikao hicho kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Kwanza hicho kuyafanyia kazi yale yote yaliyoafikiwa katika kikao cha ngazi ya Makatibu Wakuu.
Kwa upande Wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma alishauri elimu ya Muungano iendelee kutolewa hususan kwa kundi la vijana.
Alishauri kuwatumia wasanii mbalimbali nchini katika kutoa elimu ya Muungano, kwani wengi wao ni vijana hatua itakayoisaidia kufikisha ujumbe kwa haraka zaidi katika kundi hilo.
Halikadhalika, Mhe. Hamza alitoa rai kwa watendaji kutoka Ofisi hizo mbili kutangaza zaidi fursa zinazopatikana katika Muungano badala ya changamoto akisema kuwa Serikali zote zinazishughulikia ili kuzimaliza.
Awali akizungumza wakati wa kikao cha ushirikiano ngazi ya Makatibu Wakuu, Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bw. Ilyasa Pakacha Haji alisema kuwa kuna haja kubwa ya kuendeleza ushirikiano huo kukabiliana na athari za mazingira.
Alisema athari za mazingira hususan mabadiliko ya tabianchi yanagusa dunia na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo zinakumbwa na changamoto hiyo.
Hivyo, vikao vya ushirikiano ni hatua nzuri ya kuandaa na kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa ngazi ya Makatibu Wakuu, kisha kufuatilia na kufanya tahmini kutambua ni zipi changamoto na kuzifanyia kazi.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...