Na Fatma Jalala
Licha ya Tanzania kuwa na mfumo madhubuti wa kisheria unaolenga kulinda na kukuza ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma, ushahidi kutoka ngazi ya jamii unaonesha kuwepo kwa pengo kubwa kati ya kile kinachoahidiwa kupitia sera na uhalisia unaotokana na utekelezaji wa ahadi hizo.
Ukosefu wa elimu ya kutosha, unaelezwa kuwa ndio chanzo kikuu cha hali hiyo inayowakabili wajasiriamali kutoka makundi maalum, hususan wanawake.
Ingawa sheria inataka kutengwa kwa kiwango maalum cha ununuzi wa umma kwa kila taasisi kwa ajili ya makundi maalum, hilo halifanyiki na kuwanyima wajasiriamali hao kunufaika na fursa zinazopatikana kupiyia ununuzi wa umma.
Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuinua makundi maalum kiuchumi kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma, ambayo inaelekeza kutengwa kwa asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi wa umma kwa ajili ya makundi hayo. Lengo ni kuwapa fursa ya kupata zabuni, kukuza biashara ndogo ndogo, na hatimaye kuimarika kiuchumi.
Pamoja na kuwepo kwa sera na sheria hizo kwa muda mrefu, wanawake wengi katika Wilaya ya Kinondoni hawana uelewa wa kutosha kuhusu fursa hizo. Hali hiyo inasababisha kutowasilisha maombi ya zabuni, kushindwa kufikia vigezo vinavyohitajika, na hivyo kushindwa kunufaika na fursa zilizopo.
Mfumo wa kisheria na kikanuni
Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 ndiyo msingi mkuu wa taratibu za ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi kwa taasisi za serikali. Sheria hii, pamoja na kanuni zake, inasisitiza umuhimu wa kutoa fursa maalum kwa makundi yaliyoainishwa.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 64(1–2)(c), taasisi zote za ununuzi wa umma zinatakiwa kutenga angalau asilimia 30 ya thamani ya ununuzi wao wa mwaka kwa makundi maalum, yakiwemo wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wazee.
Aidha, Kanuni ya 30C ya Kanuni za Ununuzi wa Umma inaeleza umuhimu wa namna makundi maalum kusajiliwa na kuthibitishwa kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Manunuzi (NeST) ili kuzipata fursa hizo.
Kwa mujibu wa mwongozo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), mgawanyo huo wa asilimia 30 unakwenda kwa wanawake (asilimia 10), watu wenye ulemavu (asilimia 10), vijana (asilimia tano) na wazee (asilimia tano).
Changamoto ya uelewa ngazi ya jamii
Pamoja na sheria kuweka vigezo hivyo, kanuni na miongozo iliyo wazi, bado kuna changamoto kubwa ya uelewa miongoni mwa wanawake wilayani Kinondoni.
Baadhi ya wanawake wajasiriamali katika masoko ya Tandale na Magomeni wanasema hawajawahi kusikia wala kuelimishwa kuhusu mfumo wa NeST.
Kwa maana hiyo, hawafahamu fursa za ununuzi wa umma zilizotengwa kwa ajili yao.
Blandina Daniel (46), mama lishe na mweka hazina katika Soko la Tandale, anasema wanawake wengi hawajawahi kupata elimu kuhusu mfumo wa NeST wala ununuzi wa umma. Anaeleza kuwa waliwahi kuhamasishwa kuunda vikundi na kupata wataalamu kutoka BRELA, lakini jitihada hizo hazikuendelea na vikundi vikavunjika.
Theresia Paschal Joseph (44), mjasiriamali katika Soko la Magomeni, anasema maisha ya ujasiriamali yamekuwa yakitegemea mapato ya kila siku bila matarajio ya kupanua biashara kutokana na kukosa taarifa na fursa. Anaamini kuwa kama angepata elimu na uwezeshaji kupitia mifumo ya serikali, maisha yake yangekuwa tofauti.
Hali hii inaonyesha wazi kuwa tatizo kubwa si ukosefu wa sera au sheria, bali ni changamoto ya utekelezaji wa sheria hiyo hasa katika eneo la utoaji wa elimu kwa walengwa.
Kauli hizi zinaakisi uhalisia wa makundi maalum ambayo yanalindwa kisheria, lakini hayajafikiwa kielimu, hali inayodhoofisha dhamira ya sheria.
Athari za kijamii na kiuchumi
Delfina Ladslaus (38), mfanyabiashara wa mboga mboga katika Soko la Magomeni, anaeleza kuwa mara nyingi wanaambiwa kuhusu mikopo ya asilimia 10, lakini wanapoamua kufuatilia wanaishia kwenye hatua ya usajili bila kunufaika.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyu, hali hii ina athari za kisaikolojia kwao.
Kwa upande mwingine, kauli za viongozi kwamba “kinamama wamewezeshwa” wakati uhalisia ni tofauti, husababisha kukata tamaa na kupoteza imani kwa serikali.
Mariam Tandu Kimea (52) anabainisha kuwa kukosa elimu na fursa huathiri zaidi wanawake, hasa wajane na wale wanaolea familia peke yao.
Hali hii husababisha kushindwa kumudu gharama za maisha kama ada za watoto na hivyo kuendeleza mzunguko wa umaskini.
Mitazamo ya viongozi wa ngazi za msingi
Baadhi ya viongozi wa ngazi za mitaa na kata pia wanaonesha kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu mfumo wa NeST.
Diwani wa Kata ya Tandale, Abdulaziz Said (45), anasema hajawahi kupata taarifa rasmi kuhusu elimu ya mfumo huo.
Mwenyekiti wa Soko la Tandale, Sultani Kiyumbo (58), naye anasema fursa hizo anazifahamu kwa juhudi binafsi, lakini hajawahi kuona elimu ikitolewa sokoni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Soko la Magomeni, Daudi Dolle (64), anasema wanawake wengi hawajawahi kufikiwa na fursa hizo kutokana na kukosa elimu ya mfumo huo.
Uwepo wa sheria bila elimu ya utekelezaji
Kanuni za Ununuzi wa Umma, 2024 (GN Na. 518/2024), pamoja na miongozo ya PPRA, zinaweka mifumo ya uwazi, ushindani na upendeleo kwa makundi maalum. Pia, Sera ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi inalenga kutumia ununuzi wa umma kama chombo cha kuinua wanawake kiuchumi.
Hata hivyo, ripoti ya utendaji ya PPRA 2020-21, inayolezea tathmini ya utengaji wa asilimia 30 kupitia ukaguzi imebaini kuwa mambo ya msingi yaliyoainishwa kwenye sheria hayatekelezwi ipasavyo.
Sheria ya Ununuzi wa Umma inaitaka kila taasisi kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum yaani wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu. PPRA ilifanya ukaguzi ili kupima endapo taasisi hizo zilitekeleza matakwa hayoya sheria.
Ukaguzi huu ulibaini kuwa kati ya taasisi 86 zilizofanyiwa tathmini, ni taasisi mbili tu zilizozingatia matakwa haya, taasisi tatu zilikuwa zimetenga pungufu ya asilimia 30, wakati taasisi 81 hazikuwa zimetenga chochote kwa ajili ya makundi maalum.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, akizitaka taasisi za umma kutumia kikamilifu mfumo wa ununuzi wa umma kielektroniki (NeST) akisisitiza kuwa “mifumo haina mbadala.”
Naye Afisa Ununuzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Vumilia Tigwela, anakiri kuwepo kwa changamoto ya elimu na ufuatiliaji. Anasema sababu kuu ni pamoja na ukosefu wa mafunzo maalum, kampeni hafifu za uelimishaji, na changamoto za kiufundi katika matumizi ya mfumo wa NeST.
Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Halmashauri ilifanya ununuzi wa takribani shilingi bilioni 50, ambapo wastani wa shilingi bilioni mbili pekee ziliwanufaisha makundi maalum.
Wajibu wa taasisi
Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Vicky Mollel, anasema mamlaka hiyo inafuatilia utoaji wa elimu kupitia Halmashauri mbalimbali.
Hata hivyo, changamoto kubwa ni mwitikio mdogo wa walengwa na ukosefu wa ufuatiliaji wa mafunzo yanayotolewa.
Uhalisia unaonesha kuwa makundi maalum yanaendelea kubaki kuwa watazamaji wa sera zinazowahusu, badala ya kuwa washiriki.
Hali hiyo inahatarisha lengo la ununuzi wa umma kama chombo cha uwezeshaji wa kiuchumi na maendeleo jumuishi.
Bila uwekezaji mkubwa katika elimu ya mfumo wa NeST na fursa za ununuzi wa umma, dhamira ya sheria na sera zilizopo itaendelea kubaki kwenye maandishi badala ya kubadilisha maisha ya wananchi.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...