
Dkt. Arnold Koresha, Mratibu wa programu ya SafeCare, akizungumza katika hafla hiyo, leo Februari 18,2026 Dar es Salaam.
Rais wa Jukwaa la afya Tanzania (Tanzania Healthy Summit ) Dkt Omary Chillo akihutubia wakati wa hafla fupi ya kukabidhi cheti cha utoaji huduma Bora kwa hospitali ya Qualitas iliyopo Kigamboni Dar es salaam. Hafla ya kukabidhi cheti hicho imefanyila leo Februari 18, 2026 hospitalini hapo. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa hospitali hiyo Josephat Kibwana na kushoto ni mratibu wa programu ya SafeCare Dkt. Arnold Koresha.
RAIS wa Taasisi ya Afya ya Tanzania Health Summit (THS), Dkt. Omary Chilo, ametoa wito kwa watoa huduma za afya nchini kufanya tathmini ili kubaini mapungufu waiyonayo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kufikia viwango vya kimataifa.
Dkt Omary Chillo, ametoa wito huo leo Februari 18, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi cheti cha ubora cha SafeCare ngazi ya nne (Level 4) kwa Kituo cha Afya cha Qualitas kilichopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Amesema jukumu la taasisi hiyo ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya nchini, kufikia watoa huduma mbalimbali na kuhimiza taasisi hizo kuboresha huduma zao.
Akizungumzia utafiti walioufanya, Dkt. Chilo amesema wamebaini changamoto kubwa zilizopo katika utoaji huduma ni utawala, miundombinu ya kutolea huduma na utendaji wa wafanyakazi kuwa bado ni mbovu.
Amesisitiza kuwa umuhimu wa watoa huduma na vituo vya afya kufanya tathmini za mara kwa mara ni ili kubaini mapungufu yaliyopo na kuyafanyia kazi kwa lengo la kufikia viwango vinavyotakiwa.
Alieleza kuwa ubora unapaswa kuzingatiwa katika hospitali na vituo vyote vya afya, bila kujali tofauti ya huduma wanazotoa.
“Ubora unatakiwa uzingatiwe katika hospitali na vituo vyote vya afya. Siyo kwamba hospitali moja iwe bora zaidi kuliko nyingine, huduma zinaweza kutofautiana lakini ubora unapaswa kuwa uleule,” amesema Dkt Chillo.
“Tunatamani watu wote watoe huduma katika ubora wa juu zaidi. Natoa wito kila kituo kufanya tathmini ya huduma wanazozitoa ili kujua mapungufu waliyonayo,” alisema.
Amesema taasisi hiyo ipo katika sekta ya afya kwa ajili ya kutoa cheti cha ubora wa juu wa huduma za afya.
Aidha, alisema SafeCare ni programu inayofanya tathmini ya utoaji wa huduma za afya katika hospitali, zahanati na kliniki zinazotoa huduma hizo na kwamba programu hiyo ambayo inatekelezwa kimataifa ipo Tanzania kwa zaidi ya miaka 10 na imekuwa chachu ya kuimarisha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali ya Qualitas, Dkt Jane Manyahi, amesema wanafurahia kupokea cheti cha ubora wa ngazi ya nne wakiwa na uhakika wa usalama kwa wagonjwa na watoa huduma.
Amesema huduma wanazozitoa ni rafiki na zinatolewa kwa wakati.
“Napendekeza hospitali binafsi kujiunga na huduma hizi za kupima ubora kwani inaonesha uwezo wao wa kutoa huduma, mapungufu na miongozo ya kuondoa changamoto hizo,” amesema.
Aidha amewashauri watoa huduma wa sekta binafsi kujiunga na mifumo ya kujipima ubora wa huduma wanazotoa. Pia aliishauri hospitali za umma na binafsi kuzingatia viwango vya kimataifa ili kutoa huduma salama na zenye ubora.
Amebainisha kuwa kufuata viwango hivyo kunasaidia watumishi kufanya kazi katika mazingira bora na salama, jambo linaloongeza uaminifu kwa wagonjwa na jamii kwa ujumla.
“Ni jambo jema kwani linaongeza imani kwa jamii inayowazunguka, wakijua kuwa huduma wanazopata ni salama na bora,” amesema Dkt. Manyahi.
Naye mkazi wa Kigamboni, Esther Medson, aliyefika hospitalini hapo kupata huduma, ameeleza kuridhishwa kwake na huduma alizopata na kuipongeza hospitali hiyo kwa kustahili cheti cha ubora wa ngazi ya juu.
Aidha, amezitaka taasisi za sekta ya afya kuendelea kuwahudumia wagonjwa kwa weledi na kutumia taaluma zao ipasavyo ili kuboresha zaidi huduma wanazotoa.




.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...