Na MASHAKA MHANDO, Tanga

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea kwa majonzi makubwa kifo cha nguli wa muziki wa dansi nchini, Hayati Stephen Hiza (80), aliyetunga na kuimba wimbo wa kitaifa wa uzalendo, "Tanzania Nchi ya Furaha."

Hayati Mzee Hiza amehifadhiwa leo, Februari 18, 2026, katika nyumba yake ya milele eneo la Mwanzange, jijini Tanga. Akiwa na historia iliyotukuka, Mzee Hiza atakumbukwa kwa utunzi wake uliotikisa Radio Tanzania (RTD) mwaka 1967 akiwa na bendi kongwe ya Atomic Jazz ya Tanga, akizalisha vibao vilivyodumu vizazi na vizazi kama "Leo Nakupasulia", "Hamida Wangu", na "Sitamani Kitu".

Alama ya Mwaka 1967 na Uzalendo

Wimbo uliompa heshima ya kipekee na kumfanya atambulike kama "Mzalendo Namba Moja" wa sanaa ni "Tanzania Nchi ya Furaha". Wimbo huu, uliotungwa miaka sita tu baada ya Uhuru, umekuwa utambulisho wa amani na furaha ya Watanzania, jambo ambalo Rais Samia amesema litaacha alama isiyofutika.


Salamu za Pole na Tuzo ya Rais

Akizungumza kwa niaba ya Rais, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), amesema Rais Dkt. Samia aliguswa na mchango wa Mzee Hiza kiasi cha kutoa zawadi ya Shilingi Milioni 50 pamoja na tuzo ya heshima kupitia Tanzania Music Awards (TMA) mwaka 2024.

"Mzee Hiza ni kielelezo cha wasanii waliotumia vipaji vyao kujenga taifa. Rais aliipokea kwa furaha ajenda ya kumtuza Mzee Hiza kwa sababu anaijua thamani ya kazi yake tangu enzi za Atomic Jazz," alisema MwanaFA.

MwanaFA na Ahadi ya Rekodi

MwanaFA amesimulia kwa masikitiko kuwa katika tamasha la 'Hale Festival' mwishoni mwa mwaka jana, Mzee Hiza alimweleza kuwa ana nyimbo mpya alizomtungia Rais na alikuwa na shauku ya kuzirekodi. "Niliahidi kumgharamia kurekodi kwa fedha zangu, lakini Mungu amempenda zaidi kabla ya kutekeleza dhamira hiyo," alisema Naibu Waziri huyo.

Rambirambi na Heshima za Mwisho

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amethibitisha kuwa Rais Samia ametuma rambirambi ya Shilingi Milioni 20 kupitia kwa Msaidizi wake wa Kijamii, Tido Mhando

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu (MCC), Ustadh Rajab Abdalrahaman, pamoja na Meya wa Jiji la Tanga, Muhina Mustapha 'Seleboss', wameeleza kuwa pengo la Mzee Hiza halitazibika kwani alikuwa muumini wa muziki wa maadili na malezi kwa jamii.

Mzee Stephen Hiza amefariki akiwa na umri wa miaka 80, akiiacha Tanga na Tanzania katika simanzi, lakini akituachia urithi wa sauti yake ya dhahabu inayotuambia: "Tanzania, Tanzania, nchi yenye furaha...".















Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...