Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Njombe.

WAKALA wa Nishati Vijijini(REA) umetoa ruzuku ya Sh.Bilioni 1.63 kwa ajili ya kuwezesha kutekelezwa kwa mradi wa kuzalisha umeme wa maji kilowati 360 wa Ijangwala uliopo katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe ambapo umeme huo umeingzwa katika gridi ya Taifa.

Uwepo wa mradi huo wa kuzalisha umeme uliopo Kijiji cha Masisiwe, Kata ya Ukwama wilayani Makete unasimamiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT)Dayosisi ya Kusini Kati-Makete baada ya kubuni mradi huo kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya kukosa umeme katika Kanisa hilo na hivyo kutumia mafuta ya dizeli katika kufanya shughuli mbalimbali za kanisa hilo.

Akizungumza leo Machi 10,2026 mbele ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ambao ni Wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF),Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA Mhandisi Emmanuel Yessaya amesema fedha ambazo zimetolewa na wakala huo ndizo zimewezesha ujenzi wa miundombinu ya mradi huo wa umeme.

Mhandisi Yessaya amewaeleza Wahariri hao walioko katika ziara ya kutembelea mradi inayosomamiwa au kufadhili na REA,amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya uzalishaji umeme inayoungwa mkono na serikali ili kuongeza uzalishaji wa nishati bora.

“Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini REA imetoa fedha yaruzuku ya Sh. bilioni 1.63 ambazo zimetumika katika kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya mradi huu ambao kwa sasa unazalisha umeme kilowati 360 ambao unachangia umeme katika gridi ya Taifa.

“Umeme unaozalishwa katika mradi huu umesaidia kwa kiwango kikubwa hapa Wilayani Makete kuwa na umeme wa uhakika.Na kwa Mkoa wa Njombe REA tumefanikishwa kutekelezwa kwa miradi mitano ukiwemo mradi wa umeme wa Ijangwala.”

Aidha amesema Serikali kupitia REA imekuwa ikitoa ruzuku kwa waendelezaji wa miradi ya nishati kuanzia hatua za awali za maandalizi,kugharamia tafiti za awali za uwekezaji kama upembuzi yakinifu, tathmini ya athari za mazingira na maandalizi ya mpango wa biashara.

Pia amesema kupitia Mpango wa Upanuzi wa Umeme Vijijini Tanzania (TREEP), mradi huo ulipata mkopo wa Sh.milioni 922 kwa ajili ya kusaidia shughuli za utekelezaji wake.

“Baadhi ya miundombinu iliyogharamiwa na serikali ni transfoma chochezi ya KVA 500 na njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 0.6 inayounganisha kituo cha mradi na gridi ya taifa.

Awali Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Ijangala, Daud Sanga, amesema sehemu kubwa ya fedha za ujenzi wa mradi huo zimetoka REA na ukweli REA imekuwa msaada mkubwa katika kuutekeleza mradi ambao tayari umeanza kutoa matunda kwa kuuza umeme katika gridi ya taifa na kupata fedha.

Akieleza zaidi amesema miundombinu yote ya mradi huo imekamilika, ikiwemo jengo la kuzalisha umeme, bwawa la maji, mabomba ya kusafirisha maji na kituo cha kupoza umeme.

“Tunashukuru REA kwani tangu mwanzo wa mradi mpaka sasa tumekuwa pamoja katika kila hatua.Kwa kipekee tunaishukuru serikali chini ya uongozi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika,”amesema Sanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) Deodatus Balile amepongeza kazi kubwa inayofanywa na REA katika kuendelea kutekeleza miradi ya nishati ya umeme vijijini.

“REA wanafanyakazi nzuri sana wameweza kupeleka umeme katika vijiji na kweli hawa REA wanaweza kupewa hata miradi ya maji wakaipeleka vijijini kama walivyofanya kwenye umeme na hilo linawezekana maana katika umeme huku wamefanikiwa sana.”

Balile ameongeza pia ushirikiano kati ya TEF na REA kwa sehemu kubwa unasaidia jamii ya Watanzania kupata taarifa sahihi kuhusu miradi ya nishati inayotekelezwa vijijini.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...