Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao kimeendelea kuimarisha utendaji wa vyama vyake vya msingi (AMCOS) kwa kukabidhi pikipiki 32 kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa wakulima katika Wilaya za Lindi na Kilwa.

Ugawaji huo umefanyika wakati wa mkutano mkuu wa tisa wa chama hicho kwa mwaka 2025/2026 uliofanyika katika ofisi zake zilizopo Mitwero, Manispaa ya Lindi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ufanisi katika shughuli za ushirika.

Akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa chama hicho, Nurdin Said Swalla, alisema mpango huo unalenga kuhakikisha vyama vyote 61 vilivyopo chini ya chama kikuu vinapatiwa vitendea kazi hivyo, hasa vile vilivyokamilisha ulipaji wa hisa, ili kuviwezesha kuwahudumia wakulima kwa ufanisi zaidi.

Baadhi ya vyama vilivyonufaika na mgao huo wa pikipiki ni pamoja na Mnali, Ng’apa, Pachani, Mtua, Nyango, Mnolela, Matandu, Navanga, Somanga, Nachunyu na Milola.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, ameipongeza chama hicho kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi, akieleza kuwa katika msimu wa 2025/2026, zao la korosho limeingiza zaidi ya shilingi bilioni 101, ufuta zaidi ya bilioni 33, huku mbaazi zikiingiza zaidi ya bilioni 3.

Ametumia fursa hiyo kuzihimiza AMCOS za Wilaya za Lindi na Kilwa kuzingatia misingi ya ushirika na kuimarisha uendeshaji wa vyama vyao ili viwe imara kiuchumi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo, ameishukuru chama hicho kwa uwekezaji wa ghala kuu la mazao katika eneo la Hoteli Tatu wilayani humo, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa mazao kwa wakulima kutoka maghala ya AMCOS hadi ghala kuu.

Aidha, Mrajis Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Lindi, Kenneth Shemdoe, amesema uwekezaji unaofanywa na vyama vya ushirika mkoani humo unaunga mkono jitihada za serikali za kuwahudumia wakulima, huku akihimiza matumizi ya mizani za kidijitali ili kuongeza uwazi na ufanisi.

Baadhi ya wajumbe wa bodi za vyama vya ushirika walioshiriki mkutano huo wameeleza shukrani zao kwa kupatiwa pikipiki, wakisema zitapunguza changamoto ya kuwafikia wanachama na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...