Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amewahimiza wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na utamaduni wa kusaidiana katika jamii, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Eid al-Fitr.
Wito huo ameutoa wakati wa hafla maalumu ya Iftar iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, hafla iliyokwenda sambamba na harambee ya kuchangia makundi maalumu yenye uhitaji ambapo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amechangia Sh. milioni moja.
Akizungumza katika hafla hiyo, iliyowakutanisha viongozi wa serikali, viongozi wa dini na wananchi, Mhe. Nyamwese amesema kuwa Iftar hiyo imelenga kuimarisha uhusiano mzuri kati ya viongozi na wananchi pamoja na kukuza utamaduni wa kusaidiana na kushirikiana katika jamii.
Amesema mshikamano na umoja wa wananchi ni msingi muhimu katika kudumisha amani, utulivu na maendeleo ya wilaya ya Handeni, hivyo ni muhimu kila mmoja kuchukua nafasi yake katika kusaidia wenye uhitaji.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuwa na moyo wa huruma na kusaidia makundi maalumu kama yatima, wazee na watu wenye mahitaji maalumu, akisisitiza kuwa hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii.
Awali, kabla ya hafla hiyo Mhe. Nyamwese ametembelea Gereza la Wilaya ya Handeni na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wafungwa ikiwa ni kuwaonesha upendo kwao katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Eid al-Fitr.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...