Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeandaa futari maalum kwa watoto wenye uhitaji kutoka Kituo cha Kulea Watoto wenye Uhitaji cha Zili, tukio lililolenga kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuendeleza ujumuishi kwa makundi yenye mahitaji maalum.
Hafla hiyo ilifanyika katika Makao Makuu ya TCAA jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wadau wa sekta ya usafiri wa anga, watumishi wa TCAA pamoja na watoto wenye uhitaji. Wageni walishiriki futari kwa pamoja na watoto hao, pamoja na kukabidhi zawadi kama ishara ya upendo, mshikamano na uwajibikaji wa kijamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile, aliyemwakilisha Waziri wa Uchukuzi, alipongeza jitihada za TCAA katika kuchangia maendeleo ya jamii akisisitiza umuhimu wa taasisi za umma kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, hususan zinazolenga kuwajali watoto wenye uhitaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi alisisitiza kuwa pamoja na jukumu la kusimamia na kudhibiti sekta ya usafiri wa anga, mamlaka itaendelea kutekeleza miradi ya kijamii inayolenga kugusa maisha ya wananchi na kukuza maadili ya utu, mshikamano na usawa.
Kupitia futari hii maalum, TCAA imeendelea kudhihirisha kuwa sekta ya usafiri wa anga siyo tu kuhusu usimamizi na kanuni, bali pia ni chombo muhimu cha kujenga jamii jumuishi, yenye huruma na mshikamano.
Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi wakikabidhi mkono wa mwezi mtukufu kwa watoto wenye uhitaji kutoka Kituo cha Kulea Watoto wenye Uhitaji cha Zili ikiwa ni kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuendeleza ujumuishi kwa makundi yenye mahitaji maalum.
Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile akitoa neno wakati wa futari iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa TCAA, wadau mbalimbali wa Usafiri wa Anga pamoja na watoto wenye uhitaji kutoka Kituo cha Kulea Watoto wenye Uhitaji cha Zili wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na TCAA.
Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), wadau mbalimbali wa Usafiri wa Anga pamoja na watoto wenye uhitaji kutoka Kituo cha Kulea Watoto wenye Uhitaji cha Zili wakiwa kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na TCAA.
Mjumbe wa Bodi ya TCAA Vuai A. Hilal akitoa neno la shukrani kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na TCAA.



















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...