Na Mwandishi Wetu
MIRADI mikubwa ya kimkakati nchini imeonyesha tija na kuwa sehemu ya mafanikio ya kiuchumi kimataifa.
Hilo limebaimika mwishoni mwa wiki baada ya tathmini iliyotolewa na Shirika la kimataifa la Fitch Ratings Ltd lenye makazi yake New York Marekani.
Aidha, jukumu kubwa la shirika hilo ni kufanya tathmini juu ya uwezo wa nchi kuyafikia masoko ya kimataifa ya mitaji na dhamana; lakini pia kupima namna nchi ilivyo na uwezo wa kukopa na kukopesheka katika masoko ya kimataifa ya fedha.
Kupitia tathimini hiyo Fitch imeendelea kuipa Tanzania ukadiriaji wa B+ na mwelekeo wenye uthabiti ikiwa na maana uchumi wa nchi unaonekana uko katika hali ya wastani, unaendelea kukua vizuri lakini bado una changamoto fulani. “Stable” ambapo inaonyesha hali hii haitarajiwi kubadilika sana kwa muda mfupi.
Kwa upande mzuri, uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi nzuri, ukitarajiwa kufikia takriban asilimia 6 katika miaka ya 2026 na 2027 ambapo ukuaji huo unasukumwa na sekta kama kilimo na madini (hasa dhahabu).
Pia kupitia miradi mikubwa ya miundombinu kama reli ya SGR na bomba la mafuta la EACOP. Pia, mfumuko wa bei uko chini, jambo linalosaidia kulinda uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha.
Kwa upande wa fedha za Serikali, hali inaonekana inadhibitika huku nakisi ya bajeti inatarajiwa kubaki karibu asilimia 3 ya pato la taifa wakati deni la Serikali linatarajiwa kupungua kidogo.
Mapato ya kodi nayo yanaongezeka taratibu, jambo linaloonyesha juhudi za kuboresha ukusanyaji wa mapato zinaanza kuzaa matunda. Aidha, uwepo wa mpango wa IMF unaongeza imani kwa wawekezaji kuwa sera na mageuzi yataendelea.
Hata hivyo, Fitch inaonyesha changamoto kadhaa. Kwanza, mapato ya serikali bado ni madogo ukilinganisha na nchi nyingine zinazofanana na Tanzania, hali inayopunguza uwezo wa kugharamia maendeleo bila kutegemea mikopo.
Pili, bado kuna masuala ya utawala, uwajibikaji, na uimara wa taasisi, ambayo yanaathiri imani ya wawekezaji wa kimataifa.
Changamoto nyingine kubwa ni upungufu wa akiba ya fedha za kigeni (hasa dola za Marekani). Tanzania ina akiba inayoweza kufunika takriban miezi 2.5 tu ya mahitaji ya nje, kiwango ambacho ni kidogo kulinganisha na viwango vya kimataifa.
Hiyo ni hatari kwa sababu nchi inaagiza bidhaa muhimu kama mafuta na mbolea, hivyo mabadiliko ya bei duniani yanaweza kuathiri uchumi haraka. Pia, sekta ya utalii inaweza kuathiriwa na mabadiliko ya kimataifa, hasa yale yanayohusisha ukanda wa Mashariki ya Kati.
Kwa ujumla, Fitch inasema hivi:Tanzania inaendelea vizuri kwenye ukuaji wa uchumi na udhibiti wa deni, lakini bado inahitaji kuboresha ukusanyaji wa mapato, uimara wa taasisi, na usimamizi wa fedha za kigeni ili kuongeza imani na kupanda daraja zaidi.
Hata hivyo wakati wa Fitch ikitoa tathimini yake inayoonesha kuridhishwa na hali nzuri ya kiuchumi,tunafahamu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka hatua madhubuti za kuhakikisha uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika kupitia mipango na mikakati mbalimbali.
Hata hivyo Fitch inatabiri kuwa nakisi ya bajeti ya Tanzania itaendelea kuwa karibu asilimia 3 ya GDP katika miaka ya fedha inayoishia Juni 2026 na 2027, ikisaidiwa na kuimarika kwa ukusanyaji wa kodi chini ya Mkakati wa Mapato wa Muda wa Kati wa serikali.
Ukweli ni kwamba ukusanyaji mapato uliongezeka kutoka asilimia 14.2 ya GDP mwaka wa fedha 2021 hadi asilimia 15.9 mwaka wa fedha 2025, huku ongezeko zaidi likitarajiwa kusaidia matumizi makubwa katika afya, elimu, na uwekezaji wa mitaji.
Wakati deni la Serikali linatarajiwa kushuka hadi asilimia 47 ya GDP ifikapo mwaka wa fedha 2027 kutoka asilimia 50 mwaka wa fedha 2025, likibaki chini ya wastani wa nchi zenye kiwango cha B wa asilimia 54.
Hali hii inaungwa mkono na ukuaji imara wa GDP kwa thamani ya fedha na nakisi ndogo ya bajeti. Hivyo Fitch katika ripoti yake ya tathimini imeeleza kuwa asilimia 68 ya deni la Tanzania ni la nje, jambo linalofanya mwenendo wa deni kuwa hatarini kwa mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha, ingawa sehemu kubwa ya mikopo nafuu husaidia uimara wa deni.
Kwa kifupi ni kwamba Tanzania iko kwenye mwelekeo mzuri, lakini bado haijafika kiwango cha juu cha uthabiti wa kiuchumi kinachohitajika ili kupata ukadiriaji wa juu zaidi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...