Moshi, Tanzania

GGML Kili Challenge inayotekelezwa kupitia GGML Kili Trust, inashiriki Kilimanjaro Marathon 2026, maarufu kama “Mbio za Watu”, kupitia maonesho yanayofanyika katika viwanja vya Ushirika, Moshi, yaliyoanza tarehe 20 na kuendelea hadi 22 Machi. 

GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS ni mpango wa kuhamasisha ushiriki wa wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI nchini. Kupitia GGML Kili Trust, rasilimali hukusanywa na kuelekezwa kwenye miradi inayonufaisha moja kwa moja watu wanaoishi na VVU pamoja na taasisi zinazowahudumia. Mwaka huu, Kili Trust imeanza kushirikiana kwa karibu zaidi na asasi za kiraia kutoka maeneo mbalimbali nchini zinazotekeleza programu za kusaidia watu walioathiriwa na VVU na UKIMWI, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kufikia watu wengi zaidi.

Kupitia banda la GGML Kili Challenge, washiriki wa mbio na wageni wa maonesho wanapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu GGML Kili Challenge, namna ya kushiriki, pamoja na miradi inayotekelezwa chini ya mfuko huo.

Huduma za upimaji wa VVU pia zinatolewa  moja kwa moja katika banda hilo kwa kushirikiana na wadau wa kitaifa, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, kwa lengo la kuendelea kuhamasisha uelewa na hatua za kinga. Aidha, wageni wanaweza kutoa ahadi ya kuchangia, kujisajili kushiriki GGML Kili Challenge, mnamo Julai 2026, na kupata maelezo kuhusu njia mbalimbali za kushiriki katika mapambano haya.

Tangu kuanzishwa mwaka 2002, mpango huu umeendelea kuleta watu binafsi, taasisi na washirika pamoja kuchangia jitihada za kinga, tiba, matunzo na msaada kwa jamii.

Akizungumza kuhusu ushiriki huo, Meneja wa GGML Kili Trust, Stephen Mhando, amesema juhudi za mfuko huo zinalenga kuunga mkono mikakati ya taifa katika kupambana na UKIMWI kupitia ushirikiano na uhamasishaji wa jamii.

“Tunawaalika washiriki wote wa marathon na wageni wa maonesho kutembelea banda la GGML Kili Challenge ili kujifunza zaidi na kuona namna wanavyoweza kushiriki, iwe kama mtu binafsi au taasisi, katika kuunga mkono jitihada hizi.”

Kupitia ushiriki huu, GGML Kili Trust inaendelea kusisitiza umuhimu wa kufikia malengo ya sifuri tatu, yaani maambukizi mapya sifuri, unyanyapaa sifuri, na vifo vitokanavyo na UKIMWI sifuri.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...