Na Khadija Kalili, Kibaha
WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema Mkoa wa Pwani unatarajia kuanza mradi wa kilimo cha mbogamboga na matunda katika eneo lenye ukubwa wa ekari 200 lililopo Ruvu Stesheni, Kibaha Vijijini.
Akizungumza leo Machi 16, 2026 wakati akikagua eneo hilo, Mhe. Chongolo alisema ameridhishwa na mandhari ya eneo hilo na kusisitiza kuwa mradi huo utasaidia kuzalisha ajira kwa vijana wa Wilaya ya Kibaha, Dar es Salaam pamoja na wananchi wa maeneo ya jirani.
Alisema mahitaji ya mbogamboga na matunda ni makubwa katika masoko ya ndani, hivyo shamba hilo litasimamiwa na wataalamu wa kilimo watakaowaelekeza wakulima kutumia mbinu za kisasa ili kuongeza uzalishaji na tija.
“Mahitaji ya mbogamboga na matunda ni makubwa. Shamba hili litasimamiwa na wataalamu wetu ambao watawaelekeza wakulima kutumia kilimo cha kisasa ili kiwe na ufanisi na kuleta tija. Lengo ni kuhakikisha Kibaha inakuwa chanzo cha matunda na mbogamboga kwa Dar es Salaam na Zanzibar,” alisema Mhe. Chongolo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, alisema mradi huo utakuwa wa kilimo cha muda mfupi lakini chenye tija kwa jamii.
Alisema uongozi wa mkoa umefanya tathmini ya eneo hilo na kubaini linafaa kwa kilimo cha kisasa kitakachofanyika kwa mwaka mzima bila kutegemea mvua, kutokana na uwepo wa miundombinu ya umwagiliaji wa maji safi.
“Leo tumefika kufanya tathmini ya eneo hili. Kilimo kitakachofanyika hapa kitakuwa cha kisasa na cha mwaka mzima. Hatutategemea mvua kwa sababu tunayo miundombinu ya umwagiliaji wa maji safi. Tutalima mbogamboga na matunda yenye ubora,” alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa maandalizi ya awali ya mradi huo yataanza mara moja kwa kusafisha eneo hilo ili kuandaa shamba kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo.


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...