Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Njombe
MRADI wa kuzalisha umeme wa maji wa Lupali uliopo Kijiji cha Boimanda wilayani Njombe wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317 unaosimamiwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent unatarajiwa kukamilika na kuingizwa katika gridi ya Taifa ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Katika kuufanikisha mradi huo Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini(REA) imetoa ruzuku ya fedha Sh.bilioni 5.4 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya mradi huo unaokwenda kuhudumia wananchi wa Wilaya hiyo.
Akizungumza leo Machi 11,2026 mbele ya Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF)wanaotembelea miradi ya REA ,Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi wa REA Mhandisi Emmanuel Yessaya amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa umeme utakaoingizwa katika gridi ya taifa kupitia Mkoa wa Njombe.
Amefafanua tayari miundombinu ya mradi huo imekamilika na kwasasa upo hatua za mwisho kuanza uzalishaji umeme ambao utaunganishwa katika gridi ya Taifa huku akifafanua mradi huo ulibuniwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent kutokana na kukosekana umeme katika shirika hilo na vijijini jirani ingawa tayari REA imeshapeleka umeme.
“Miradi kama hii inasaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na kuchochea shughuli za kiuchumi.Nitoe rai kwa wawekezaji kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji kuanzisha miradi ya kuzalisha umeme.”
Amefafanua katika mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma kuna vyanzo vya maji vingi ambavyo vinaweza kutumika kwa ajili ya miradi ya kuzalisha umeme,hivyo ni wakati muafaka kuchangamkia fursa na REA ipo tayari kushirikiana nao.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo, Sister Imaculatha Mlowe kutoka Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent ameeleza ruzuku iliyotolewa na REA imesaidiakukamilisha ujenzi wa miundombinu ya mradi ikiwemo ujenzi wa intake weir, jengo la kuzalishia umeme,uwekaji wa mabomba ya kusafirisha maji, pamoja na kazi nyingine za ujenzi.
Pia amesema fedha iliyotolewa na REA imesaidia kugharamia tafiti za awali za mradi, ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme za msongo wa kilovoti 11 zenye urefu wa kilomita 23.48 na njia ndogo za kusambaza umeme kwa watumiaji zenye urefu wa kilomita 30.61.
“Miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme imeshakamilika na itaunganishwa gridi ya taifa kupitia TANESCO kwani tayari imefika katika kijiji jirani cha Kitulila.
“Hadi sasa wananchi zaidi ya 212 wa Kijiji cha Boimanda wameunganishwa na kupata huduma ya umeme kupitia gridi ya TANESCO wakati wananchi 366 wa Kijiji cha Matola wakipata umeme kupitia mradi wa zamani wa Lupali.”
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema mradi mradi huo unaonesha namna ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi unavyoweza kusaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.
“Uzalishaji umeme ni moja ya vigezo muhimu vya maendeleo ya taifa kwani miradi ya aina hiyo itasaidia Tanzania kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 4,031 za sasa hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.”



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...