Na Mwandishi wa OMH

Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amefanya mazungumzo na Bw. Keith Liddell, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa kampuni ya Lifezone Metals Limited, inayomiliki Tembo Nickel Corporation Limited kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mazungumzo hayo yalifanyika Jumatatu, Machi 2, 2026, katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, yakilenga kujadili maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kabanga Nickel uliopo mkoani Kagera, ambao thamani ya uwekezaji wake unakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 2.5.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya madini nchini, ukiwa na matarajio ya kuibadili Tanzania kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa madini ya nickel duniani.

Mkutano huu umefanyika katika wakati muafaka, ikizingatiwa kuwa Uamuzi wa Mwisho wa Uwekezaji (Final Investment Decision – FID) unatarajiwa kufanyika mwaka huu (2026).

Msajili wa Hazina alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unazingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na tija, huku ukitoa manufaa mapana kwa wananchi.

Bw. Mchechu alibainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji unaonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza rasilimali za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Bw. Liddell alieleza kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa katika hatua ya awali kabla ya FID, na kusisitiza dhamira ya kampuni kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika kuufanikisha mradi huo wa hadhi ya kimataifa.

Ilielezwa kuwa mradi huo unawakilisha fursa ya kipekee kwa Tanzania na kwa soko la kimataifa la nickel, hasa katika kipindi ambacho mahitaji ya madini hayo yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya nishati na ukuaji wa teknolojia za kisasa.

Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliokamilika Julai 2025, Kabanga ni miongoni mwa machimbo makubwa na yenye kiwango cha juu cha madini ya nickel sulfidi duniani yaliyo tayari kuendelezwa.

Mradi wa Kabanga unatarajiwa kuongeza thamani ya rasilimali za nickel kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uchenjuaji, kukuza ajira kwa Watanzania, kuimarisha ujuzi wa ndani, na kuongeza mapato ya Serikali pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Aidha, utekelezaji wake utaimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya madini na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa za kampuni, mikakati ya upatikanaji wa fedha inaendelea kwa mfumo wa njia nyingi (multi-track financing strategy), huku mazungumzo ya kina yakiendelea na wawekezaji wakubwa wa kimkakati, taasisi za kifedha na wanunuzi wa muda mrefu wa madini (off-takers).

Katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, Desemba 8, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, alifanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, ambapo moja ya ajenda kuu ilikuwa kuharakisha ukamilishaji wa mikataba ya uwekezaji kwa Mradi wa Kabanga Nickel pamoja na miradi mingine ya kimkakati ya rasilimali asilia inayokaribia hatua ya ufadhili.

Kwa miezi ya karibuni, mikutano na maonesho ya uwekezaji (roadshows) imefanyika Tanzania, barani Ulaya, Japan, Afrika Kusini na Marekani, ikizihusisha taasisi za mikopo ya mauzo ya nje (Export Credit Agencies – ECAs) na benki za biashara.

Mradi wa Kabanga Nickel unaendelea kuonekana kuwa nguzo muhimu katika mkakati wa Tanzania wa kuongeza thamani ya rasilimali zake za madini, kuimarisha uchumi wa viwanda, na kujipanga vyema katika soko la kimataifa la madini muhimu kwa maendeleo ya teknolojia na nishati safi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...