Na Humphrey Shao,Michuzi Tv

Dar es Salaam, Machi 2, 2026 – Serikali imetangaza kuwa kesho, Machi 3, 2026, kutafanyika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mpango mkubwa wa kupanua na kuboresha bandari hiyo kama lango kuu la biashara nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye ataongoza tukio hilo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya uchukuzi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Profesa Mbarawa amesema ujenzi wa matanki hayo unaonesha dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha miundombinu ya kimkakati itakayoongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia meli za mafuta na kuiweka miongoni mwa bandari zenye ushindani mkubwa katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi wa ujenzi wa matanki 15 unatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2027, ambapo yatakuwa na uwezo wa kupokea shehena ya mafuta ya mita za ujazo 378,000 kwa wakati mmoja. Hatua hiyo itawezesha bandari kuhudumia meli kubwa za mafuta na kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 10 hadi siku 3 kwa meli zenye ujazo wa tani 150,000.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutavutia meli nyingi zaidi za mafuta kutumia Bandari ya Dar es Salaam, kupunguza foleni ya meli, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuimarisha usalama wa nishati nchini.

Kwa sasa, bandari hiyo ina matanki yanayomilikiwa na wadau wengine yenye uwezo wa mita za ujazo 1,051,888.52. Utekelezaji wa mradi huu utaongeza uwezo wa kupokea mafuta hadi kufikia mita za ujazo 1,429,888.52, na kuifanya bandari hiyo kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Kusini, Kati na Mashariki mwa Afrika.

Sambamba na uimarishaji wa bandari, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya reli ikiwemo ukarabati wa reli ya MGR, kukamilisha ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR pamoja na kuboresha reli ya TAZARA kwa ushirikiano na sekta binafsi. Kupitia reli hizo, shehena itakayohudumiwa bandarini itasafirishwa hadi maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, hatua itakayopunguza msongamano wa mizigo bandarini na wa malori katika Jiji la Dar es Salaam, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi katika mnyororo wa ugavi.

Profesa Mbarawa amewahimiza wadau wa sekta ya uchukuzi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na vifaa vya usafirishaji ili kuongeza kasi ya uondoshaji mizigo bandarini na kuimarisha ushindani wa taifa.

Aidha, amewakaribisha wanahabari, wadau wa usafirishaji, wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani kushiriki katika tukio hilo ambalo amelitaja kuwa la kihistoria na lenye umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...