WANANCHI wa Kitongoji cha Shuleni, Kijiji cha Holili Vijijini wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia athari za maji ya mvua yaliyoelekezwa kwenye makazi yao kufuatia uchimbaji wa mitaro uliofanywa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari jana, wananchi hao  wamesema hali hiyo imeanza kuleta madhara tangu kuanza kwa mvua za masika.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Ibrahim Tarimo amesema mitaro hiyo imeelekeza maji moja kwa moja kwenye mashamba na makazi, hali iliyosababisha baadhi ya nyumba kuingiliwa na maji na hata ukuta wa uzio wa  nyumba ya mkazi mmoja kuanguka kufuatia mvua zinazonyesha hali ambayo inaleta hofu kubwa hasa kwa watoto wanaobaki nyumbani peke yao wakati wa mchana.

Kwa upande wake, Julius Lazaro amesema changamoto hiyo ilianza tangu mwishoni mwa mwaka 2025 baada ya TARURA kutengeneza barabara na kuelekeza mitaro kwenye makazi ya wananchi, hali inayowafanya wananchi kuishi kwa hofu hasa nyakati za usiku mvua zinaponyesha.

Amesema kuwa baada ya madhara hayo, waliwasilisha malalamiko yao kwa TARURA ambao walifika eneo la tukio na kuahidi kulifanyia kazi, lakini hadi sasa bado  hatua hazijachukuliwa.

“Barabara imetengenezwa vizuri, lakini changamoto ni haya maji yanayokuja moja kwa moja kwenye makazi yetu,” amesema.

Kwa upande wake, Medilaster Tarimo amesema maji hayo yameharibu mashamba na kuingia ndani ya nyumba yake, na kwamba anahofia madhara zaidi endapo mvua zitaendelea kunyesha bila hatua kuchukuliwa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Holili Vijijini, Peter Mandu alisema tayari taarifa za tatizo hilo zimefikishwa kwa TARURA pamoja na kwa mkurugenzi wa halmashauri, na kwamba mhandisi alishafika eneo hilo kujionea hali halisi. 

Ameongeza kuwa ni muhimu hatua za haraka zichukuliwe ili kuelekeza maji kwenye makorongo na kuepusha madhara zaidi.

Akizungumzia Suala hilo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Rombo, Rickson Lema amesema tayari wamefika eneo husika na kufanya ukaguzi kwa kushirikiana na wananchi na kwamba upo mpango wa kuchepusha maji hayo, lakini unahitaji makubaliano kutoka kwa wananchi hasa wamiliki wa mashamba yatakayopitishwa mtaro mpya.

“Tulishauriana na wananchi kuhusu uwezekano wa kuelekeza maji kwenye korongo. Tunawasubiri wakubaliane kupitia serikali ya kijiji ili tuanze utekelezaji wa mradi huo,” amesema Lema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...