Kuna methali isemayo “Asiyejua maana haambiwi maana “ lakini Ngorongoro leo itakuambia maana ya Nyayo za Laetoli.
Nyayo hizi ni za kihistoria na ni sehemu pekee duniani ambayo mafundi Viatu ulimwenguni wanaweza kufika na kutengeneza Viatu vya kihistoria vinavyoweza kushinda nishani ya Nobel kutokana na Nyayo za Laetoli zilivyo.
Katika eneo la Laetoli ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, tarehe 24, Julai mwaka 1978, Mtafiti maarufu wa masuala ya Akiolojia Dr. Mary Leakey na timu yake iliyomhusisha Dkt. Paul Abell waligundua nyayo za zamadamu katika eneo la Laetoli zilizohifadhika katika mwamba wa jivu la volcano inayoaminika kuwa ililipuka katika mojawapo wa milima ya Ngorongoro miaka milion 3.6 iliyopita.
Wataalamu hawa wanaamini kuwa nyayo hizo ziliachwa na jamii ya watu wa kale wanaofahamika kama Australopithecus Afarensis.
Nyayo za Zamadamu katika eneo la Laetoli ni ushahidi wa pekee na wa bayana duniani kote usiopingika kwamba zamadamu (Hominin) kwa mara ya kwanza walianza kusimama wima na kutembea kwa miguu miwili katika eneo la Laetoli Ngorongoro Tanzania miaka milioni 3.6 iliyopita.
Binadamu hawa waliotembea wima kwa miguu miwili wametokana na babu/bibi mmoja aliyeishi miaka takribani millioni 7 iliyopita.
Mwanadamu aliyepo Tandahimba, Gamboshi kule Bariadi, Tandale kwa mtogole, Mbagala Zakiem na yule aliyepo Jerusalemu, Macca, Dubai, New York, London, Johannesburg, Tehran, Gaza, Misri hadi Sudan na Mumbai wametokana na babu na bibi mmoja.
Katika kuthibitisha uhai, Nyayo za zamadamu ndizo za kustaajabisha katika eneo la Laetoli, zipo nyayo za wanyama wengine wa kale kama vile nyayo za tembo, twiga, faru na wanyama ndogo kama sungura, kanga na aina za wadudu.
Kwa nyayo za Laetoli zilivyo, mafundi Viatu na wamiliki wa viwanda vya Viatu duniani wanaweza kufika katika Eneo hilo ili kupata ujuzi zaidi wa namna ya kutengeneza Viatu vya kihistoria.
Karibu kwetu Ngorongoro ambapo kila ukilala kuna ndoto ya maajabu inakuita
Muonekano wa Nyayo za Laetoli zilizoachwa na jamii za watu wa kale wanaofahamika kama Australopithecus Afarensis




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...