Mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Mhe. Christopher Ngubiagai (aliyesimama),akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa waganga wa tiba asili na tibambadala yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu waSerikali. Mafunzo hayo yalifanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 26 hadi 27, 2026. Kulia ni Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Ziwa, John Wanjala na kushotoni Kaimu Meneja wa Maabara ya Chakula na Dawa, Everlight Matinga.
*************
Serikali kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya kuinua sekta ya tiba asili nchini baada ya kuzindua mafunzo ya uchakataji salama wa dawa asili kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala kutoka mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika Machi 26, 2026 Ukerewe, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, alisema serikali inatambua mchango mkubwa wa waganga wa tiba asili katika utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania, huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Afya inayotambua rasmi tiba asili na tiba mbadala hapa nchini.
“Serikali imewaleta wataalamu wa GCLA ili kuhakikisha dawa za asili zinachakatwa kwa viwango vinavyokubalika, zinakuwa salama na zenye ubora unaoweza kushindana hata katika masoko ya kimataifa,” alisema Ngubiagai.
Aidha, Ngubiagai Aliongeza kuwa jitihada hizo pia zinalenga kurasimisha sekta ya tiba asili na kuwajengea uwezo waganga hao ili waweze kuwa sehemu ya mfumo rasmi wa huduma za afya nchini, hatua itakayoongeza heshima na uwajibikaji wao katika jamii, ambapo pia alihusisha mafunzo hayo na Dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, akibainisha kuwa tiba asili ina mchango mkubwa katika kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora, kukuza uchumi shindani unaotumia rasilimali za ndani pamoja na kuchochea ubunifu na ajira.
Katika hatua nyingine, Ngubiagai alisisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya uchakataji salama ikiwemo usafi wa mazingira ya utayarishaji, matumizi ya vipimo sahihi vya dawa, ufungashaji bora pamoja na ushirikiano na wataalamu wa afya ili kuepuka madhara kwa watumiaji huku akiweka wazi kuwa tiba asili inaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato kupitia biashara na hata utalii wa tiba endapo ubora wake utaimarishwa na kuwekewa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
Akimwakilisha Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, Meneja wa Kanda ya Ziwa, John Wanjala, alisema kuwa lengo la Mamlaka ni kuhakikisha dawa zote zinazozalishwa zinakuwa salama, bora na zenye uwezo wa kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi huku akieleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwasaidia waganga wa tiba asili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ikiwa ni pamoja na kuboresha uzalishaji na kupanua masoko ya bidhaa zao.
“Popote walipo waganga wa tiba asili, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali tutaendelea kuwafikia kwa mafunzo na huduma za kitaalamu ili kuhakikisha wanatoa huduma zilizo bora na salama kwa jamii,” alisema Wanjala.
Kwa upande wake Katibu wa chama cha Tiba Asili na Tiba Mbadala (TAMESOT), Maneke Malegeli, akizungumza kwa niaba ya washiriki, aliishukuru Mamlaka kwa mafunzo hayo kwa kuwa yamewasaidia kupata uelewa wa mbinu bora za utengenezaji, utayarishaji na ufungashaji wa dawa asili kwa kuzingatia viwango vinavyolinda afya za watumiaji na kuongeza kuwa mafunzo hayo pia yatawasaidia kujitofautisha na matapeli wanaotumia jina la tiba asili vibaya, huku pia akiiomba Mamlaka kuendelea kutoa elimu hiyo ili iweze kuwafikia waganga wengi zaidi nchini.
Waganga wa tiba asili na tiba mbadala kutoka Ukerewe, wakimsikilizamgeni rasmi (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo hayo ya siku mbili.
Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Ziwa, John Wanjala, akiwasilisha mada kuhusu mbinu bora za uzalishaji na usafi wa dawa za tiba asili kwenye mafunzo yaliyofanyika Ukerewe, mkoani Mwanza.

Mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Mhe. Christopher Ngubiagai (katikati), akipokea zawadi kutoka kwa Mlezi wa Waganga na Wakunga wa Tiba Asili - Ukerewe, Makubi Makubi baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mtumishi wa Mamlaka, Lulu Kiwia, akifafanua jambo kuhusu aina yauchunguzi wa kimaabara unaofanyika kwenye dawa asili wakati wamafunzo kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala yaliyofanyika wilayaniUkerewe.
Kaimu Meneja wa Maabara ya Chakula na Dawa, Everlight Matingaakiwasilisha mada kuhusu vifungashio vya dawa asili.
Mshiriki wa mafunzo, Consolata Nabina, akichangia hoja kuhusuufangushaji na uhifadhi wa dawa wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyikaUkerewe.
Katibu wa Chama cha Tiba Asili na Tiba Mbadala (TAMESOT), ManekeMalegeli, akiandika maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya (hayupopichani) wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika Ukerewe, Mwanza.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...