Na WAF - Uingereza 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuimarisha juhudi za kukuza utafiti na ubunifu katika sekta ya afya ili kukabiliana na changamoto za ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) pamoja na magonjwa ya kuambukiza. 

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Machi 16, 2026 jijini London wakati akiwasilisha taarifa ya uimarishaji wa mifumo ya afya kwa kutumia tafiti na ubunifu akiwa ziarani nchini Uingereza kwa lengo la kuendelea kuimarisha huduma za afya nchini. 

"Serikali ya Tanzania ilianzisha Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ili kuimarisha utafiti na ubunifu nchini na kukabiliana na changamoto za magonjwa," amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa tafiti zilizofanyika nchini Tanzania zimesaidia kuboresha miongozo na utaoaji wa huduma ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO) limeweza kuandaa miongozo ya tiba Duniani kupitia tafiti hizo. 

"Tafiti hizo ni zile za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ugunduzi na matibabu ya kifua kikuu kwa WAVIU pamoja na matumii ya watoa huduma ngazi ya jamii iliyosaidia kupungua kwa vifo vya watoto vijijini," amesema Dkt. Magembe 

Amesema, Tanzania imeongeza ubunifu na kupelekea Dunia kujifunza kupitia ubinifu huo wa mifumo ya usimamizi wa taarifa za afya kwa kutumia teknolojia za kidijitali ambapo Mkakati wa Afya Kidijitali wa Tanzania wa mwaka 2025–2030 unasisitiza usalama wa taarifa, ujuzi wa kidijitali pamoja na matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI) ili kuboresha matumizi ya takwimu katika tafiti na ubunifu.

"Mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa taarifa za afya ikiwemo Mfumo wa GoTHOMIS tayari umewekwa kutumika katika vituo vya afya vya msingi, huku mfumo wa AFYA-HMS ukiwa umefungwa katika hospitali zote 28 za Rufaa za Mikoa, na jitihada zinaendelea kuunganisha mifumo hiyo ili kuboresha matumizi ya taarifa," amesema Dkt. Magembe 

Mwisho, Dkt. Magembe amesema, Serikali imeanzisha mfumo wa rufaa za dharura kwa wajawazito (m-mama) kuratibu rufaa za akina mama na watoto wachanga kutoka vituo vya afya vya msingi kwenda hospitali za juu ambao umechangia kupungua kwa vifo vya akina mama kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2022," amesema Dkt. Magembe.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...