SERIKALI imetangaza mpango wa kuongeza ndege nane kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hatua itakayofikisha jumla ya ndege 24 ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usafiri wa anga na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, alipokuwa akizungumza na watumishi wa ATCL katika miji ya Cape Town na Johannesburg nchini Afrika Kusini, ambapo ameelezea kuwa shirika hilo lilianza na ndege moja mwaka 2016 na sasa lina ndege 16
Aidha, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali imeongeza ndege sita kubwa, kwa lengo la muda mfupi ni kufikia ndege 19 ndani ya mwaka wa fedha 2025/2026, kabla ya kufikia ndege 24 ifikapo mwaka 2030.
Ongezeko hilo la ndege limewezesha kupanuka kwa mtandao wa safari za ndani, ambapo kwa sasa ATCL inahudumia miji mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Mtwara, Kigoma, Iringa, Pemba, Unguja, Songea, Mpanda, Tabora na Bukoba. Aidha, mipango ipo ya kuanza safari katika miji ya Sumbawanga, Musoma na Shinyanga hivi karibuni.
Katika ngazi ya kimataifa na kikanda, shirika hilo linaendesha safari zake katika miji ya Nairobi, Entebbe, Bujumbura, Lubumbashi, Lusaka, Harare, Johannesburg, Guangzhou (China), Mumbai (India) na Dubai, pamoja na huduma za usafirishaji mizigo (cargo) zinazochangia kukuza biashara na uchumi wa taifa.
Katika hotuba yake, Kihenzile amewahimiza watumishi wa ATCL kuendelea kufanya kazi kwa weledi, nidhamu na uwajibikaji kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, amebainisha kuwa uwepo wa ATCL katika miji ya Johannesburg na Cape Town unachochea ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini.


.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...