Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Agellah Jasmine Kairuki, amezindua rasmi mfumo wa kidijitali wa kuhudumia watumiaji wa huduma za mawasiliano ujulijanao kama Mtumiajiapp ulioandaliwa na TCRA-CCC , leo Tarehe 23/03/2024 katika ukumbi wa Millennium Towers uliopo jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau wa sekta ya mawasiliano pamoja na wananchi mbalimbali.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Kairuki alisema kuwa uzinduzi wa mfumo huo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini. Alieleza kuwa mfumo huo utasaidia watumiaji kupata taarifa muhimu, elimu ya matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano pamoja na kutoa nafasi ya kuwasilisha changamoto na maoni yao.


Waziri  Kairuki alibainisha kuwa serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024 hadi 2034 uliozinduliwa na Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkakati huo unalenga kuongeza uelewa wa matumizi ya teknolojia na kuhakikisha wananchi wanatumia mifumo ya kidijitali kwa usalama na ufanisi.


Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), idadi ya laini za simu imeongezeka na kufikia milioni 106.9 hadi Desemba 2025, huku watumiaji wa intaneti wakifikia milioni 58.6. Ongezeko hilo linaonesha kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano nchini.


Serikali pia imeendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambapo jumla ya minara 758 imejengwa na kufikisha huduma katika vijiji zaidi ya 1,400. Hatua hiyo imewezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za mawasiliano hata katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.


Pamoja na mafanikio hayo, Waziri Kairuki alitaja changamoto zinazokabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa watumiaji, uvunjifu wa faragha, pamoja na vitendo vya utapeli mtandaoni. Alisema mfumo wa Mtumiaji utasaidia kushughulikia changamoto hizo kwa kutoa njia rahisi ya kuwasiliana na wadau husika.


Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC), Bi. Mary Shao Msuya, alisema mfumo huo utarahisisha upokeaji wa maoni, utoaji wa elimu na utatuzi wa changamoto za watumiaji kwa wakati. Aliongeza kuwa mfumo huo utasaidia pia kuhifadhi taarifa kwa njia ya kidijitali na kupunguza matumizi ya karatasi.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC), Dkt. Nkundwe Mosese, pamoja na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bi. Hawa Ngh’umbi, walisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kupewa elimu ya matumizi sahihi ya teknolojia. Walieleza kuwa mfumo huo utachochea uwajibikaji, kulinda haki za watumiaji na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.










Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...