JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imesisitiza matumizi ya Akili Unde (Artificial Inteligence – AI) ikiwa ni moja ya nyenzo muhimu na ya kisasa katika kukuza mtangamano na kuharakisha maendeleo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Elimu, Viwanda, Afya na Biashara.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo katika Kongamano la Nne la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (4th EAC Regional Science, Technology and Innovation Conference) lililoandaliwa na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EASTECO) kwa kushirikiana na Bazara la Vyuo Vikuu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (IUCEA), linalofanyika jijini Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 30 Machi – hadi 1 Aprili 2026.

Waziri Kombo akizungumza katika Kongamano hilo lililowakutanisha viongozi wa ngazi za juu Serikalini kutoka nchi wanachama wa EAC, wabunifu, wanataaluma, wanadiplomasia na wadau wa maendeleo, amesisitiza nafasi ya akili unde katika kuongeza ufanisi na tija ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma za umma na kuimarisha ushindani wa kiuchumi ndani ya Jumuiya na kwenye soko la kimataifa.

Akizungumzia mchango wa Tanzania, Waziri Kombo alieleza kuwa, Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kukuza sekta za Teknolojia, Uchumi wa Kidijitali na Ubunifu kama nguzo muhimu za agenda ya maendeleo ya taifa na Dira ya Maendeleo ya 2050. Alisisitiza kuwa mwelekeo huo unalenga kuchochea maendeleo jumuishi, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuinua ustawi wa jamii hususan vijana.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Waziri Kombo amehimiza nchi wanachama kuongeza juhudi za pamoja katika utafuataji wa rasilimali fedha za kuendesha programu mbalimbali ikiwemo utafiti na ujenzi wa miundombinu ya kidijitali, kubadilishana maarifa, kukuza ubunifu wa ndani na kuendeleza miradi ya pamoja ya teknolojia ili kujenga uthabiti wa kiuchumi na kijamii katika Jumuiya.

Mbali na hayo Waziri Kombo aligusia umuhimu wa kuweka mifumo thabiti ya sera na udhibiti na utoaji elimu ili kuhakikisha matumizi salama na yenye maadili ya Akili Unde. Aliongeza kuwa pasipo kuwa na usimamizi madhubuti wa teknolojia hiyo inaweza kuongeza changamoto katika jamii ikiwemo tishio la usalama na kukithiri kwa tofauti ya kiuchumi.

Katika mkutano huo uliofanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Matumizi ya Akili Unde kwa ajili ya Afrika Mashariki yenye Ustahimilivu, Jumuishi na Ubunifu” (“Harnessing Artificial Intelligence for a Resilient, Inclusive and Innovative East Africa”) ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo aliyeambatana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Kaimu Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Said Shaib Mussa, Maafisa Waandamizi wa Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na Wanataaluma kutoka Taasisi za mbalimbali za Elimu ya Juu nchini.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...