Na Mwandishi Wetu, London

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametangaza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji wa kimataifa katika kukuza Sekta ya Afya na Sayansi , akisisitiza kuwa taifa linaelekea kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya barani Afrika.

Akizungumza leo jijini London kwa niaba ya Waziri Mchengerwa kwenye Jukwaa la Uwekezaji la Afya na Sayansi ikiwa ni jitihada za Serikali za kuleta mageuzi makubwa katika uwekezaji wa viwanda vya ndani vya uzalishaji wa bidhaa za afya na vifaa tiba Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia eneo la Dawa na vifaaa tiba Emmanuel Tayari amewahakikishia wawekezaji dhamira ya dhati ya Serikali ya kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji kufanya uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa Tiba nchini Tanzania.


Jukwaa hiyo limeratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza na Wizara ya Afya ambapo Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki na upande wa Wizara Dkt. Seif A. Shekalaghe, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Emmanuel Tayari Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Dawa na Vifaa Tiba, Dkt. Grace Magembe Mganga Mkuu wa Serikali wamehudhuria. Aidha, wwngine ni Watendaji kutoka TISEZA, TMDA, MSD, MUHAS pamoja na wataalam wa Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Dawa (PIAT) nchini.


Alibainisha kuwa juhudi hizo zinaungwa mkono kikamilifu na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye anaipa kipaumbele ajenda ya uwekezaji katika afya kama sehemu ya kuimarisha usalama wa afya, maendeleo ya viwanda na ushirikiano wa kimkakati.


Katika hotuba yake, Mchengerwa alieleza kuwa Tanzania sasa inaiona sekta ya afya si tu kama huduma ya kijamii, bali pia kama injini ya ukuaji wa uchumi. “Tunataka kuwa zaidi ya soko la bidhaa za afya zinazoagizwa kutoka nje. Tunataka kuwa kitovu cha uzalishaji, ubunifu na usambazaji wa kikanda,” alisema.

Alisisitiza kuwa uzoefu wa janga la UVIKO-19 umeonesha umuhimu wa nchi kuwa na uwezo wa ndani wa kuzalisha dawa, chanjo na vifaa tiba, akionya kuwa utegemezi mkubwa wa uagizaji kutoka nje unaweza kuhatarisha upatikanaji wa huduma muhimu wakati wa dharura.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania imeweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, ikiwa ni pamoja na uthabiti wa uchumi, idadi kubwa ya watu zaidi ya milioni 65, na mageuzi ya mfumo wa bima ya afya yatakayosaidia kuongeza mahitaji ya huduma za afya kwa utaratibu unaotabirika.

Aliongeza kuwa nafasi ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inaipa nchi faida ya kipekee ya kuhudumia soko kubwa la kikanda, jambo linalovutia zaidi wawekezaji.

Katika hatua ya kuimarisha sekta hiyo, serikali inaendelea kuendeleza Eneo Maalum la Kiuchumi la Dawa la Mloganzila pamoja na vituo vya uzalishaji wa dawa katika maeneo ya Mloganzila na Kibaha. Pia imeanzisha Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Dawa (PIAT) kwa lengo la kurahisisha taratibu na kuharakisha uwekezaji wa kimkakati.



Mchengerwa alisisitiza kuwa Tanzania haitaki kuwa soko la teknolojia zilizopitwa na wakati au bidhaa duni, bali inalenga uzalishaji wa dawa za kisasa zinazokidhi viwango vya kimataifa. “Dawa duni hugharimu maisha. Hatuwezi kuendelea kuwa soko la dawa za jana wakati dunia imeendelea,” alionya.

Alihimiza wawekezaji kuangalia fursa zilizopo katika uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, uchunguzi wa magonjwa, mifumo ya usambazaji, pamoja na utafiti na maendeleo ya rasilimali watu.

Kwa upande wake, alisema Uingereza ina nafasi muhimu katika kushirikiana na Tanzania kutokana na uzoefu wake katika teknolojia ya afya, utafiti na uwekezaji, akikaribisha ubia wa kimkakati utakaosaidia kukuza sekta hiyo.



Akihitimisha, Waziri Mchengerwa alitoa wito kwa wawekezaji wa kimataifa kuchangamkia fursa zilizopo nchini Tanzania, akisisitiza kuwa serikali iko tayari kuwezesha mazingira bora ya uwekezaji.

“Fursa ipo, soko linakua, na dhamira ni thabiti. Tunakaribisha wawekezaji kushirikiana nasi kujenga mustakabali wa afya barani Afrika,” alisema.

Katika Jukwaa hilo pia Meneja wa Biashara na Maendeleo, Philip Conradi wa Kampuni kubwa Duniani ya uzalishaji wa Bidhaa za Afya- Sartorius alihudhuria.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...