NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) itaendelea kutoa fursa za mafunzo endelevu ya viongozi wa elimu wa ngazi mbalimbali na wadau wengine wa elimu ili waweze kuimarisha uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule kwa ajili ya utoaji wa elimu bora nchini.

Ameyasema hayo Mkurugenzi wa Elimu msingi, Abdul Maulid wakati akimwakilisha Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir katika ufungaji mafunzo ya uongozi, usimamizi na utawala bora wa elimu kwa Maafisa Elimu Kata Tanzania Bara yaliyofanyika katika Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), katika Halmashauri ya Bagamoyo, mkoani Pwani.

Amesema mafunzo hayo yamekusudiwa kuwajengea uwezo viongozi na wasimamizi wa taasisi za elimu ili waweze kusimamia ipasavyo rasilimali na michakato ya utoaji wa elimu, huku wakizingatia misingi ya uongozi bora, uwazi na uwajibikaji.

"Ni matumaini yetu kuwa, ADEM mtaendelea kutoa mafunzo yanayoelenga kuimarisha uongozi, usimamizi na uendeshaji wa elimu kwa njia endelevu na yenye mafanikio pamoja na kufanya tafiti mbalimbali zakielimu na kutoa ushauri wa kitaalam katika masuala ya uongozi. Ninawasihi muendelee kufanya kazi kwa weledi ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa ADEM". Amesema

Ameongeza kuwa ushirikishwaji wa jamii, matumizi sahihi ya takwimu za elimu na utoaji wa fursa za mafunzo endelevu kwa walimu ni mambo muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu.

Ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa waliyoyapata kuboresha utendaji wao, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa weledi, ubunifu, kujituma na uzalendo ili kufanikisha malengo ya sekta ya elimu nchini.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid amesema kuwa mafunzo hayo yametekelezwa kama sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa elimu kwa kuzingatia misingi ya uongozi bora, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za elimu.

"Mpango huu ulianza kwa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu Wakuu wa shule za msingi kuhusu Uongozi, Usimamizi na Utawala Bora wa Elimu, yaliyowahusisha Walimu Wakuu 17,817 kutoka Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara". Amesema

Amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwaimarisha Walimu Wakuu katika kusimamia shule kwa kutumia mbinu stahiki za uongozi pamoja na kuzingatia sera, miongozo na viwango vya kitaifa ili kuhakikisha kuwa shughuli za ufundishaji na ujifunzaji zinafanyika kwa ubora, ufanisi na kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

Pamoja na hayo Dkt. Maulid amesema kuwa tathmini inaonyesha kiwango kikubwa cha mabadiliko ya kiutendaji kwa walimu wakuu katika kuongoza na kusimamia shule zao baada ya kupatiwa mafunzo hayo.

`












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...