
Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ahmed akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 13, 2026 katika hafla ya futari kwa Waislam na Wakristu iliyoandaliwa na TCD kwa wadau wa demokrasia na vyama vya siasa.
Na Mwandishi Wetu.
KITUO cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimeendelea kuimarisha juhudi za kuvikutanisha vyama vya siasa nchini kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa na kukuza utamaduni wa majadiliano unaochochea demokrasia, amani na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 13, 2026 katika hafla ya futari kwa Waislam na Wakristu iliyoandaliwa na TCD kwa wadau wa demokrasia na vyama vya siasa, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ahmed, alisema majadiliano ya wazi na vikao vya pamoja kati ya vyama vya siasa ni muhimu katika kujenga demokrasia imara na kuimarisha utulivu wa nchi.
Alisema Tanzania imeendelea kujitofautisha na mataifa mengine kwa kudumisha amani na utulivu, akibainisha kuwa misingi hiyo inalindwa na utamaduni wa kuvumiliana na kushirikiana licha ya tofauti za kisiasa.
“Watanzania tunapaswa kuendelea kulinda amani yetu kwa kutumia majukwaa ya mazungumzo na maridhiano. Njia zinazoweza kuhatarisha utulivu wa nchi hazina nafasi katika jamii yetu,” alisema Ahmed.
Awali, Mwenyekiti wa TCD, Dorothy Semu, alisema taasisi hiyo ina jukumu la kuvikutanisha vyama vya siasa ili kujadiliana masuala muhimu ya kisiasa na kitaifa licha ya tofauti za kiitikadi na kimtazamo.
Alisema mfumo wa vyama vingi unatoa nafasi ya kushindanisha mawazo na sera mbalimbali kwa lengo la kupata suluhisho bora kwa maendeleo ya taifa, huku akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kutafsiriwa kama uadui bali fursa ya kujifunza na kuboresha mifumo ya uongozi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Miraj Mtibwiriko, alisema pamoja na kuwepo kwa vyama vingi na mitazamo tofauti ya kisiasa, ni muhimu kwa Watanzania kuendelea kudumisha umoja wa kitaifa kwa kuwa lengo la vyama vyote ni kuboresha maisha ya wananchi.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Salum Mwalimu, alisema chama hicho kimejiunga na TCD baada ya uchaguzi wa mwaka 2025 na kimejipanga kushirikiana kikamilifu katika kukuza demokrasia nchini.
Alisema TCD imekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mazungumzo ya kisiasa na kutoa elimu kwa vyama vya siasa kupitia makongamano, semina na mafunzo mbalimbali.
TCD ni taasisi inayovikutanisha vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, katika mabaraza ya madiwani na Baraza la Wawakilishi kwa lengo la kukuza demokrasia, haki na amani nchini kupitia majadiliano na ushirikiano wa wadau wa kisiasa.

.jpeg)
.jpeg)
Matukio mbalimbali katika picha.




.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...