.jpeg)
Waziri wa Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 9,2026 wakati wa ufunguzi wa kongamano la kujadili nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre).
SERIKALI imetaja ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) kuwa nyenzo muhimu itakayochochea utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini, huku ikisisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za kiuchumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la kujadili nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), Waziri wa Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa.
Amesema serikali inatarajia zaidi ya asilimia 70 ya fedha za utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano zitatoka katika sekta binafsi kupitia uwekezaji na miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, mpango huo unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2026/2027 umeweka malengo mbalimbali, ikiwamo kuimarisha uthabiti wa uchumi, kuboresha miundombinu ya usafiri na kuongeza tija katika sekta za uzalishaji.
Amesema ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuwa na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi kwa kuwa serikali pekee haiwezi kutekeleza shughuli zote za kiuchumi.
“Jukumu la serikali ni kuweka sera, sheria na kusimamia uchumi kwa ujumla, lakini shughuli nyingi za kiuchumi zinaweza kutekelezwa kwa ufanisi zaidi na sekta binafsi,” amesema.
Aidha, amesema Tanzania pia imejiwekea malengo makubwa ya kukuza uchumi katika kipindi cha miaka 25 ijayo kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuongeza ukubwa wa uchumi hadi kufikia zaidi ya dola trilioni moja za Marekani.
Ameongeza kuwa tayari baadhi ya miradi imeanza kutekelezwa kupitia mfumo wa PPP katika sekta mbalimbali ikiwamo usafiri, miundombinu na huduma za biashara, huku mingine ikiwa katika hatua tofauti za maandalizi.
Hata hivyo, amekiri kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya PPP bado ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya miradi iliyopangwa, hali inayolazimu serikali kuendelea kuboresha mifumo ya kisheria na kiutendaji ili kuongeza ufanisi.
Amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuhamasisha taasisi za umma kutumia mfumo wa PPP pale ambapo miradi inaweza kutekelezwa kwa ufanisi zaidi kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kuratibu ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha miradi inayoweza kutekelezwa kwa ubia inatekelezwa kwa ufanisi.
Amesema kongamano hilo ni mwanzo wa majadiliano ya mara kwa mara yatakayokuwa yakifanyika kila mwezi kwa lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwamo wanazuoni, wataalamu wa uchumi, sekta binafsi na taasisi za serikali ili kujadili masuala ya maendeleo ya uchumi na utekelezaji wa miradi ya ubia.













Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...