
Mchakato wa kumwaga lami katika barabara ya Kahama-Kakola inayojengwa kwa uwezeshaji wa kampuni ya Barrick nchini ukiendelea

Mchakato wa kumwaga lami na kuisambaza ukiendelea

Msimamizi wa Ujenzi wa barabara ya Kahama-Kakola kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Marco Bee, akiongea kuhusu maendeleo ya ujenzi huo unaotekelezwa kwa ufadhili wa kampuni ya Barrick nchini.

Msimamizi Msaidizi kutoka kampuni ya Barrick, Mhandisi Ibahim Paul akielezea maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
**
#Wafikia hatua ya barabara kuwekwa lami
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kahama-Bulyanhulu JCT- Kakola kwa kiwango cha lami yenye kilomita 73 kwa uwezeshaji wa migodi ya Barrick nchini ya Bulyanhulu na North Mara yenye ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals kwa gharama ya shilingi bilioni 101.2 umefikia hatua ya kuwekwa lami na kudhihirisha dhamira ya kampuni ya uwekezaji unaoenda sambamba na kufanikisha miradi mikubwa endelevu inayobadilisha maisha ya wananchi kuwa bora na itakayoacha alama ya kudumu hadi kwa vizazi vijavyo.
Kutekelezwa kwa mradi huu mkubwa unaojengwa na kampuni ya China Civic Engineering Construction Corporation ni kielelezo kinachodhihirisha ubia wa Barrick na Twiga unavyofanikisha kuchochea utengenezaji endelevu wa thamani katika uchumi wa Tanzania na jinsi Serikali ikishirikiana na sekta binafsi inavyoweza kuleta matokeo Chanya kwa kufanikisha miradi mukubwa endelevu inayoweza kunufaisha wananchi kwa kipindi kirefu.
Akiongea kuhusu maendeleo ya mradi Msimamizi wake mkuu kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Marco Bee, alisema ujenzi unaendelea vizuri na kazi inayofanyika kwa sasa hivi ni kuweka lami kwenye Barabara na aliongeza kuwa kazi iliyofanyika mpaka sasa ni sawa na asilimia 65 ambapo mradi ulianza mwezi Julai 2024.
“Kazi inaendelea kwa kasi nzuri licha ya changamoto za hali ya hewa ya mvua,mkandarasi anafanya vizuri na naamini anaweza kumaliza kazi hii ndani ya kipindi cha miezi 27 iliyobainishwa katika mkataba ikizingatiwa kuwa kampuni ya Barrick inayofadhili mradi huu inatoa fedha za kufanyia kazi kwa wakati,”alisema Mhandisi Bee.
Mhandisi Bee, alisema kukamilika kwa barabara hii itakuwa ni fursa ya kufungua milango ya kiuchumi nchini na inafungua milango kwa wawekezaji na wafanyabiashara wazawa pia ni moja ya mikakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Naye Msimamizi Msaidizi kutoka kampuni ya Barrick, Naye Mhandisi Ibahim Paul, alisema kwamba ujenzi wa barabara hii umetekelezwa kwa weledi kwa kuzingatia taratibu na ubora ili itakapokamilika iwe alama ya kudumu kama moja ya miundombinu bora inayowanufaisha wananchi moja kwa moja kutokana na uwekezaji wa kampuni ya Barrick kupitia migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara kwenye eneo lao kwa kuwafungulia milango ya kujikwamua kiuchumi na kuwaunganisha na maeneo mengine kwa urahisi.
Hatua hii iliyofikiwa inaendelea kushuhudiwa na kuwapatia faraja wananchi wanaoishi katika maeneo hayo ambao wanakumbuka kabla ya ujenzi miaka hadi miaka barabara hiyo ilikuwa ni moja ya kero kubwa ya muda mrefu kutokana na kuwa katika hali mbaya wakati wote iwe kipindi cha mvua ama kipindi cha kiangazi.
Akiongea kwa niaba ya baadhi ya wananchi wanaotumia barabara hiyo waliokutwa eneo ka ujenzi , Mkazi wa kakola , Mwandu John, alisema kabla ya ujenzi kwa miaka mingi barabara hiyo imekuwa ni kero kubwa kutokana na kuwa katika hali mbaya wakati wote iwe kipindi cha mvua ama kipindi cha kiangazi ambapo ilisababisha kuharibika kwa vyombo vya usafiri na kuongeza gharama za maisha kutokana kupoteza muda mrefu kutoka Kahama Kwenda Bulyanhulu.
“Tunashukuru kampuni ya Barrick nchini kwa kufanikisha mradi huu mkubwa wa ujenzi wa Barabara hii kwa kiwango cha lami,mradi huu utanufaisha vizazi na vizazi sambamba na kufungua fursa za biashara na uwekezaji kwenye eneo hili letu na kutuunganisha na miji mingine kwa kweli tunajivunia sana ujenzi wa barabara hii,” alisema Mwandu.
Kwa upande wake mkazi wa Kakola,Hamis Mabubu alisema “Tunayo furaha kubwa kuona barabara hii inatengenezwa kwa kiwango cha lami ambapo mbali na kurahisisha maisha itasaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo haya yaliyokuwa yanafifishwa na ubovu wa miundombinu.Tunawashukuru Barrick kwa kuendelea kudhihirisha kwa vitendo kama mdau mkubwa wa maendeleo katika wilaya ya Kahama,Msalala na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.
Naye Samwel Petro akiongea kwa niaba ya madereva wa vyombo vya moto wanaotumia barabara hiyo alisema kwa muda mrefu ubovu wa barabara unawasababishia hasara kubwa ya kuharibika kwa vyombo vyao ila anaamini sasa ujenzi ukikamilika tatizo hilo litaisha na fursa za biashara zitaongezeka maradufu na kufungua milango ya ajira kwa vijana.
Kukamilika kwa barabara hii ambayo ilianza kujengwa mnamo mwezi Julai mwaka juzi kutafungua fursa za kiuchumi za madini, Kilimo, Misitu na Utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma.
Pamoja na Barabara hiyo kufungua fursa za kiuchumi za madini, kilimo, misitu na utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma mara baada ya kukamilika pia barabara hiyo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Mkoa wa Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama ambako kuna mkusanyiko mkubwa wa Wasafirishaji wa mizigo kutoka bandari kuu ya Tanzania kwenda nchi za jirani za Rwanda na Uganda.
Mkakati endelevu wa kampuni ya Barrick unabainisha kuwa Uchimbaji madini ukifanyika kwa umahiri ni nguvu kubwa ya kuleta maendeleo na Jamii zinazoishi kwenye maeneo ya shughuli zake zikipata mafanikio ni mafanikio yake pia.


Mchakato wa kumwaga lami na kuisambaza ukiendelea

Mchakato wa kumwaga lami na kuisambaza ukiendelea

Mchakato wa kumwaga lami na kuisambaza ukiendelea









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...