Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kusimamia na kukamilisha mradi wa kupeleka umeme wa gridi mkoani Kigoma na hivyo kuokoa takribani shilingi bilioni 58 zilizokuwa zikitumika kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa mafuta na matengenezo ya vipuri vya majenereta ya kuzalisha umeme.

Mhe. Salome ametoa pongezi hizo tarehe 6 Machi 2026 mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa kituo kikubwa cha Kupoza umeme cha Kidahwe kilichopo mkoani Kigoma pamoja na kituo cha kupoza umeme cha kigoma mjini na kituo cha muda cha Kidahwe.

“Niwapongeze TANESCO kwa kufikisha umeme wa gridi Kigoma hasa baada ya kukamilisha mradi kutoka Nyakanazi hadi Kigoma na kwa kuamua kutumia fedha zenu za ndani shilingi bilioni tano kukamilisha kituo cha muda cha Kidahwe ambacho kwa sasa kinapeleka umeme Kigoma wakati ujenzi wa kituo kikubwa cha umeme Kidahwe ukiendelea,” amesema Mhe. Salome

Amesema kituo kipya cha umeme cha Kidahwe kitakuwa na uwezo wa megawati 192 na hivyo kitaimarisha zaidi hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Kigoma ambao kwa sasa unapata takribani megawati 30.

Ameongeza kuwa kituo hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu na kitasaidia pia kuimarisha hali ya umeme katika mikoa ya Magharibi, kuendesha Treni ya Mwendo Kasi (SGR) pamoja na kuchochea biashara ya umeme na nchi jirani za Magharibi mwa Tanzania.

Kutokana na uwepo wa umeme wa kutosha mkoani Kigoma, Mhe. Salome amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika mkoa huo.

Aidha, amewaasa wananchi kulinda miundombinu ya umeme akieleza kuwa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya nishati nchini hivyo wananchi wanao wajibu wa kuilinda na kuithamini.

Awali, Mratibu wa Mradi wa Kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma, Mhandisi Ramadhan Uwessu, alisema kuwa ujenzi wa kituo kipya cha Kidahwe unaenda sambamba na upanuzi wa kituo cha Nyakanazi ili kukiwezesha kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Nyakanazi hadi Kidahwe.

Ameongeza kuwa kituo hicho pia kitapokea umeme kutoka njia ya Tabora kwa msongo wa kV 132, kutoka Sumbawanga kwa msongo wa kV 400 pamoja na umeme utakaozalishwa kutoka mradi wa Malagarasi.

Amesema mradi huo umefikia asilimia 47 ya utekelezaji na unagharimu takribani shilingi bilioni 434 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na Mfuko wa Maendeleo wa Watu wa Korea Kusini (EDCF).










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...