Na: OWM (KAM) - Mwanza
Serikali imehimiza wananchi kujiunga katika na Hifadhi Skimu ili kujihakikishia usalama wa maisha yao ya sasa na baadaye ikiwemo kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Akizungumza katika hafla ya uhamasishaji wa kujiunga na hifadhi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amewasihi wananchi kutumia fursa hiyo kujiunga kwa wingi na kuchangia kikamilifu ili wanufaike na mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu pamoja na mafao ya uzeeni.
Aidha, amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa NSSF imeanzisha Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi waliojiajiri kwa ajili ya kuhudumia Wananchi waliojiajiri kwenye shughuli za kiuchumi.
Waziri Sangu amebainisha kuwa Hifadhi Skimu ni mpango wa uchangiaji wa hiari unaolenga kuwafikia wananchi waliojiajiri wakiwemo wavuvi, wafanyabiashara, machinga, bodaboda, wakulima, wachimbaji wadogo, wasanii pamoja na makundi mengine yanayounda sehemu kubwa ya nguvu kazi ya Taifa.
Vilevile, amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mazingira rafiki ya ajira na kujiajiri sambamba na kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika kunufaika na huduma hizo muhimu.
“Hifadhi ya jamii ni haki ya msingi inayosaidia wananchi kuwa na maisha yenye heshima hasa wanapofikia umri wa uzee au wanapokumbana na changamoto zisizotarajiwa kama vile maradhi” amesema.
Awali akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewahimiza wananchi wa Mkoa wa huo kuchangamkia fursa ya kujiunga na Hifadhi Skimu, akieleza kuwa ni hatua muhimu ya kuilinda familia dhidi ya majanga ya maisha pamoja na kujihakikishia kipato cha baadaye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Masha Mshomba amesema Hifadhi Skimu itawasaidia wananchi kuboresha maisha yao kwa kuondokana na utegemezi, hivyo kuwawezesha kujitegemea kiuchumi na kupata usalama wa maisha yao si tu kwa sasa bali pia wanapofikia umri wa uzee.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...