Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
KWA muda mrefu mjadala wa matumizi ya uzazi wa mpango umeonekana kuwa wa wanawake pekee. Kliniki nyingi za afya ya uzazi hujaa wanawake huku wanaume wakibaki pembeni, kana kwamba suala hilo halihusiani nao.

Hata hivyo, uzoefu wa baadhi ya wanaume unaonyesha kuwa ushiriki wao unaweza kubadilisha kabisa ustawi wa familia kuanzia afya ya mama hadi hali ya kiuchumi ya nyumbani.

Heri Abeid ni mwanaume anayeshiriki kikamilifu katika matumizi ya uzazi wa mpango kwa kushirikiana na mwenza wake, akieleza uamuzi huo haukutokana na shinikizo la nje bali tathmini ya hali halisi ya maisha yao.

Abeid ambaye ni mkazi wa Mapinga Bagamoyo anasema “Tuliona kulea watoto kwa mpangilio ni bora kuliko kupata watoto mfululizo bila maandalizi. Kupanga uzazi kunasaidia familia kuwa na utulivu na malezi bora kwa watoto tulionao."

Anasema hali ya uchumi wa familia na afya ya mwenza wake ndiyo vilikuwa vichocheo vikuu vilivyowafanya waanze kufikiria kupanga uzazi.

Katika familia nyingi, maamuzi ya uzazi wa mpango yanaweza kuibua mijadala mikali au hata migogoro. Lakini kwa wanandoa hawa, mazungumzo ya wazi yalikuwa hatua ya kwanza kabla ya kufika kituo cha afya kupata ushauri wa kitaalamu.

Anasema walifika katika kituo cha afya kinachosimamiwa na Wizara ya Afya ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu njia mbalimbali za uzazi wa mpango.
Baada ya maelezo kutoka kwa wahudumu wa afya, waliamua kutumia njia ya sindano ambayo mwenza wake hupata katika kituo cha afya, na wakati mwingine walitumia kondomu kama njia ya ziada ya kujikinga.

“Tulichagua njia hii kwa sababu ni rahisi kufuatilia na kwa mujibu wa ushauri wa daktari, haikuwa na athari kubwa kiafya kwa mwenza wangu,” anaeleza.

Mbali na faida za kiafya, Abeid anasema uzazi wa mpango umeleta mabadiliko makubwa katika usimamizi wa mipango ya familia.

“Sasa tunaweza kupanga matumizi, kuwekeza kidogo na kuhakikisha watoto tulionao wanapata mahitaji yao vizuri. Hakuna presha ya majukumu mapya bila maandalizi,” anasema.
Kwa mtazamo wake, uzazi wa mpango si suala la afya pekee bali pia ni nyenzo ya kusaidia familia kujijengea uthabiti wa kiuchumi.

Afya ya Mama na Ustawi wa Watoto Abeid anafafanua uamuzi wa kupanga uzazi pia umeleta nafuu katika afya ya mwenza wake kwamba nafasi ya kupumzika kati ya ujauzito mmoja na mwingine imeimarisha afya yake na kumpa muda wa kurejesha nguvu.

“Watoto wanapata muda wa uangalizi na mahitaji yao yanatimizwa vizuri zaidi. Tunakuwa na muda na nguvu za kuwalea vizuri,” anasema.

Licha ya faida hizo, takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya uzazi wa mpango bado yako chini nchini. Tafiti mbalimbali za afya ya uzazi zinaonyesha kuwa chini ya nusu ya wanawake walio katika ndoa hutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, huku matumizi ya jumla yakikadiriwa kuwa karibu asilimia 35.

Wataalamu wanasema moja ya sababu kubwa ni ushiriki mdogo wa wanaume katika maamuzi ya uzazi ndani ya familia.

Mtaalamu mwandamizi wa masuala ya afya ya uzazi, jinsia na familia, Dkt. Katanta Simwanza, anasema kwa muda mrefu programu nyingi za uzazi wa mpango zililenga zaidi wanawake kuliko wanaume.
“Mpaka sasa matumizi ya njia za uzazi wa mpango yako chini ya asilimia 35 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo mitazamo ya kidini, dhana potofu na ukosefu wa usawa wa jinsia katika maamuzi ya familia,” anasema.

Anaongeza kuwa wanaume walipaswa kutambuliwa kama wenza na wateja wa huduma hizi tangu mwanzo.

“Tunafahamu mwanaume mmoja anaweza kusababisha mimba nyingi kwa muda mfupi, wakati mwanamke anaweza kubeba ujauzito mara moja kwa mwaka. Hivyo ni muhimu programu za afya ya uzazi kuwahusisha wanaume kikamilifu,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Dkt Simwanza, uzazi wa mpango unasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuboresha afya ya familia na kutoa nafasi kwa wazazi kujenga ustawi wa kiuchumi.

Changamoto za kijamii bado zipo Abeid anasisitiza si kila mtu katika familia au jamii alikubaliana na uamuzi wao kwani baadhi ya ndugu waliamini kuchelewesha kupata watoto ni kama kuchelewesha baraka.

“Kulikuwa na maneno kutoka kwa baadhi ya ndugu, lakini tulisimama kwenye uamuzi wetu kwa sababu tunajua hali yetu ya maisha na malengo yetu,” anasema.
Changamoto kama hizi zinaonyesha jinsi mitazamo ya kijamii bado inaathiri maamuzi ya wanandoa kuhusu uzazi wa mpango.

Juma Said, mkazi wa Dar es Salaam ambaye hatumii uzazi wa mpango, anaeleza sababu kuu ya kutofanya hivyo ni hofu na mitazamo aliyoikulia katika jamii.

“Mimi binafsi bado nina wasiwasi kuhusu madhara ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango. Pia katika familia yetu tunaamini watoto ni baraka, hivyo ni vigumu kupanga idadi yao,” anasema.

Anasema pia wanaume wengi hawapati taarifa za kutosha kuhusu njia zinazowahusu moja kwa moja.

“Ukienda hospitali utakuta wanawake wengi. Wanaume wengi tunaona kama hili ni jambo la wanawake, hivyo hatujiingizi sana,” anaeleza.

Wito kwa wanaume Abeid anasema kushiriki katika uzazi wa mpango ni sehemu ya uwajibikaji wa mwanaume katika familia.

“Kupanga uzazi si kupunguza uanaume ni kuonyesha uwajibikaji kwa familia yako na familia yenye mpangilio huleta utulivu na heshima kwa wenza,” anasema.

Wataalamu wa afya wanaamini kuwa kadiri wanaume watakavyoanza kushiriki zaidi katika maamuzi ya uzazi, ndivyo familia nyingi zitakavyoweza kupanga maisha yao kwa utulivu zaidi kuanzia afya ya mama na mtoto hadi ustawi wa uchumi wao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...