Na Said Mwishehe,Michuzi TV

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limetembelea mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji sita vilivyopo ukanda wa Ziwa Nyasa wilayani Ludewa mkoani Njombe, mradi unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kiasi cha fedha Sh. bilioni 3.1.

Utekelezaji wa mradi huo ulianza kutekelezwa Julai 13, mwaka 2025 na unatarajiwa kukamilika Aprili 13, 2026, ukilenga kuwapatia huduma ya umeme wateja wa awali takribani 160 na kisha Shirika la Umeme Tanzania(TNESCO) litaendelea kuunganisha umeme kwa wateja kwa gharama ile ile ya Sh.27000.

Msimamizi wa Miradi wa REA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Dastan Kalugira, amewaambia Wahariri wa Jukwaa hilo leo Machi 12,2026 kwamba mkandarasi wa mradi huo, Suma JKT, tayari amekamilisha kazi ya kusimamisha nguzo zote 105 zinazohitajika katika vitongoji vyote vinavyonufaika na mradi huo.

“Hatua iliyobaki ni kuvuta waya ili kukamilisha miundombinu ya usambazaji wa umeme kabla ya wananchi kuanza kupata huduma hiyo.Mradi huu ni wa kipekee kutokana na mazingira ya milimani katika eneo hilo, hali iliyosababisha changamoto katika usafirishaji wa vifaa na utekelezaji wa kazi.”

Kalugira amevitaja Vitongoji vitakavyonufaika na mradi huo ni Kitewele na Kimata vilivyopo wilayani Ludewa, pamoja na Kigulu, Chanjale, Lumbira na Nkanda ambavyo vinapata umeme kutoka Matema wilayani Kyela mkoani Mbeya.

Awali Msimamizi wa mradi huo, Yassin Seleman, kutoka SUMA JKT amesema utekelezaji wa mradi ulikumbwa na changamoto kutokana na mazingira ya eneo hilo la kijiji cha Madunda ambako mradi unatekelezwa ikiwemo milima mikali na hali mbaya ya hewa hasa mvua.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, ameendelea kuwapongeza REA kwa kutekeleza miradi ya umeme vijijini.“Leo tunashuhudia vitongoji sita vilivyopo katika mazingira magumu vikielekea kupata huduma ya umeme. Tunawapongeza REA kwa kazi hii nzuri ambayo inafanya katika kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosha.”

Pamoja na hayo REA imesema Mkoa wa Njombe, kuna jumla ya vijiji 381 na vyote tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme. Kati ya vitongoji 1,833 vilivyopo mkoani humo, vitongoji 1,249 tayari vimepata umeme.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...