-Asema taasisi za dini nguzo ya maadili na amani nchini
-Aonya migogoro ya ardhi inaweza kuvuruga mshikamano wa Taifa
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini nchini katika kulinda amani, kuimarisha maadili na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumapili (Machi 15, 2026) wakati akitoa salamu katika Ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mpanda Mjini, Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, iliyoongozwa na Askofu Imani Ahobokile Chibona.
Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika kujenga Taifa lenye hofu ya Mungu, upendo, haki na uwajibikaji.
“Nimekuja pia na salamu za upendo kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye anatambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika kudumisha amani, maadili mema na mshikamano wa kitaifa,” amesema.
Waziri Mkuu amesema taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, hususan katika sekta za elimu, afya na malezi ya jamii.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Katavi ikiwemo miradi ya maji, barabara na nishati kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumzia sekta ya maji, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 ambapo jana aliweka jiwe la msingi la mradi wa kusambaza maji kutoka Bwawa la Milala unaotarajiwa kuzalisha lita milioni 12 za maji kwa siku na kuhudumia wakazi wa Manispaa ya Mpanda.
Katika sekta ya miundombinu, amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya Mpanda – Tabora yenye urefu wa kilometa 352 kwa kiwango cha lami ambayo imekuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo.
Aidha, amesema ujenzi wa barabara ya Mpanda – Uvinza – Kanyani unaendelea ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 15.7, huku ujenzi wa barabara ya Kagwira – Karema nao ukiendelea kwa lengo la kufungua fursa za kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Waziri Mkuu pia amesema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme katika Mkoa wa Katavi ambapo vijiji vyote 172 tayari vimeunganishwa na umeme huku vitongoji 534 kati ya 912 vikifikishiwa huduma hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa akisisitiza kuwa amani ya nchi ni matokeo ya jitihada za pamoja za Serikali, taasisi za dini na wananchi.
“Taifa letu limeendelea kuwa kisiwa cha amani kwa sababu ya mshikamano wa Watanzania. Tuendelee kuwa mabalozi wa amani katika familia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa mnufaika namba moja wa amani ni mwananchi mwenyewe na Taifa kwa ujumla.
“Tunapaswa kuepuka migogoro isiyo ya lazima hususan ya ardhi. Hata tukigombana au kupigana ardhi haiongezeki. Kilicho muhimu ni kukaa pamoja, kuzungumza na kushirikishana ili kutumia ardhi yetu kwa manufaa ya wote,” amesema.
Amesema kuendelea kwa migogoro ya ardhi kunaweza kuliweka Taifa katika mazingira yasiyo mazuri na kupelekea chuki pamoja na kuvunjika kwa umoja wa kitaifa. Ameongeza kuwa msingi wa maendeleo ya Taifa lolote ni amani, umoja na mshikamano, hivyo ni muhimu kuendelea kuliombea Taifa lisipoteze tunu hizo.
Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Dkt. Imani Ahobokile Chibona, amesema Kanisa linaendelea kuhimiza waumini kudumisha amani, mshikamano na maadili mema katika jamii kwani amani ya Taifa inaanza na mtu mmoja mmoja katika familia na jamii.
Askofu Chibona pia ameitaka jamii kuendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa ili Mungu awape hekima, nguvu na afya njema katika kuliongoza Taifa, huku akisisitiza kuwa Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...