-Asisitiza amani na kuishi kindugu
WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amewaomba Wabunge wa Mbulu na uongozi wa wilaya hiyo waendelee kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuendeleza amani na kuishi kindugu.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Machi 2, 2026) wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye hospitali ya Lutheran ya Haydom, wilayani Mbulu, mkoani Manyara mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la afya ya mama na mtoto.
“Nimepata taarifa ya kuwepo kwa mizozo kule Yaeda Chini. Waheshimiwa Wabunge wa majimbo haya mawili na viongozi wa Halmashauri kaeni na wananchi muwaelimishe kuwa ardhi haiongezeki. Kaeni na wananchi muwaeleze kuwa suluhisho ni kupanga matumizi bora ya ardhi.”
“Endeleeni kuwaelimisha wananchi kuwa hata wakipigana ardhi haiongezeki. Hata mkiwaondoa kabila fulani, bado ardhi haiongezeki kwa sababu watu wanaendelea kuzaa.”
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa jengo hilo, Waziri Mkuu amesifu kazi nzuri iliyofanywa na akamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya hospitali zinazoendeshwa na taasisi za dini ili kuboresha utoaji huduma kwenye hospitali hizo.
“Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alielekeza taasisi zinazotoa huduma kwa jamii (charitable organisations) zipewe nafuu ya kikodi. Hii ni kwa sababu hizi taasisi hazifanyi biashara na serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na hizo taasisi,” amesema.
Akitoa maelezo kuhusu fedha zinazotolewa na serikali kwenye hospitali hiyo, Naibu Waziri – OWM-TAMISEMI (Elimu), Reuben Kwagilwa alisema kumekuwa na ushirikiano wa mrefua ambapo kila mwezi, Serikali imekuwa ikilipa sh. milioni 188 kwa ajili ya watumishi 128 wa hospitali hiyo.
“Serikali pia imekuwa ikitoa ruzuku ya sh. milioni 545 kila mwaka ambazo hupitia MSD kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba. Vilevile, imekuwa ikitoa sh. milioni 57 kila mwaka kwa ajili ya uendeshaji wa hospitali,” amesema.
Mapema, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mbulu, Askofu John Nade alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanashukuru kwa ushirikiano uliopo baina ya Serikali na kanisa kwenye utoaji wa huduma za jamii.
Alisema mbali na hospitali, wana Taasisi ya Afya ya Haydom ambayo inatoa mafunzo kwenye kozi tano ambazo ni Radiolojia, Famasia, Afisa Tabibu, Maabara na Uuguzi.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Haydom, Dkt. Paschal Mdoe alisema ujenzi wa jengo hilo umegharimu sh. bilioni 6.3 ambazo zimetokana na vyanzo vya ndani na marafiki wa Haydom Norway.
Alisema hospitali hiyo ya Kanisa imekuwa mdau mkubwa na wa muda mrefu katika sekta ya afya, ikitoa huduma za rufaa na kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na mikoa jirani, pamoja na kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya ya jamii.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...