Na Diana Deus-  Kagera.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imezindua rasmi vituo 23 vya kukusanyia maziwa (Milk Collection Centers – MCCs) vilivyojengwa na kuboreshwa kupitia Mradi Shirikishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa Tanzania (TI3P).

Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, alisema mradi wa TI3P unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika mnyororo wa thamani wa maziwa nchini kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kupanua masoko kwa wafugaji wadogo, wa kati na wakubwa. Alisisitiza kuwa vituo vya kukusanyia maziwa si majengo tu, bali ni miundombinu ya kimkakati inayochochea mapinduzi ya kiuchumi kwa wafugaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza ajira vijijini.

Alisema Mkoa wa Kagera uliwahi kupiga hatua kubwa kwa kujikita katika masuala ya ushirika kabla ya kudorora, na kufufua ushirika kupitia sekta ya ufugaji ni njia muhimu ya kuinua uchumi wa kaya na kuurudishia mkoa hadhi yake ya kiuchumi kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Aidha, aliwashauri wafadhili wa mradi wa TI3P ambao ni Gates Foundation pamoja na watekelezaji ambao ni TADB kwa kushirikiana na Heifer International Tanzania na Land O’Lakes Venture 37 kuendelea kuimarisha ushirikiano huo wenye lengo la kuwaunganisha wazalishaji na wasindikaji ili kukuza sekta ya maziwa kwa njia jumuishi na endelevu kupitia mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa.”

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, alisema hadi sasa zaidi ya Shilingi bilioni 41 zimetolewa kama mikopo kwa wadau katika mnyororo wa thamani wa maziwa.

Mradi umewezesha ununuzi wa mitamba 3,254 yenye thamani ya Shilingi bilioni 10.8 kwa lengo la kuongeza uzalishaji, pamoja na ufadhili wa viwanda 15 vya usindikaji maziwa kwa Shilingi bilioni 22.

Zaidi ya wafugaji 92,831 watafikiwa moja kwa moja kupitia huduma za kifedha, mafunzo na ugani. Ruzuku fungamanifu ya Shilingi bilioni 1.448 imetolewa kwa wafugaji na wasindikaji wa maziwa, huku Vyama vya Wazalishaji wa Maziwa (FPOs) 45 vikianzishwa na kuimarishwa, vikikusanya wastani wa lita 19,047 kwa siku.

Vituo 23 vya kukusanyia maziwa vimejengwa na kuboreshwa katika Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar, vyenye uwezo wa kukusanya lita 45,500 kwa siku na kuhudumia wafugaji 4,016 katika mikoa nane na wilaya 18, kwa uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 1.157.

Katika ziara yake mkoani Kagera, Waziri alitembelea Chama cha Ushirika cha Maruku, Bukoba Mjini, na kushuhudia utekelezaji wa mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa” unaolenga kuongeza kipato kwa vijana na wanawake kupitia ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa.

Chama hicho chenye wanachama 118, kati yao asilimia 26 ni wanawake, kimewanufaisha wanachama 24 waliopatiwa mitamba 24 yenye mimba. Pia wamepata ruzuku ya Shilingi milioni 18 kupunguza marejesho ya mikopo, ukarabati wa MCC wa Shilingi milioni 10.4 na tanki la kuhifadhia maziwa la lita 2,000. Wanachama hao wamepatiwa pia mbegu bora za malisho aina ya Juncao na mafunzo ya ufugaji bora kutoka Heifer International Tanzania.

Katika Kituo cha Nshamba chenye wanachama 541, kati yao wanawake 83, TADB imewezesha uanzishwaji wa MCC yenye uwezo wa kukusanya lita 2,000 kwa siku pamoja na jenereta ya dharura. Wanachama 143 wako katika mchakato wa kunufaika na mpango huo kwa kupatiwa mitamba 45 yenye mimba.

Aidha, katika Ushirika wa UWAWAMA, Kayanga wilayani Karagwe, wanachama 76 wamenufaika na mpango huo kwa kupatiwa mitamba 110 yenye mimba na ruzuku ya Shilingi milioni 85 ya kupunguza marejesho ya mikopo.

Kwa upande wa usindikaji, Mkurugenzi wa Kahama Fresh, Josam Ntangeki, alisema TADB imeendelea kushirikiana na Kahama Fresh Limited tangu Oktoba 2021 kwa kuwezesha ujenzi wa kiwanda na ununuzi wa mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kusindika lita 20,000 za maziwa kwa siku pamoja na magari maalum ya kukusanya na kusambaza maziwa.

Alisema mwaka 2024, kupitia mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa,” benki iliwezesha upatikanaji wa mitamba bora kutoka Kenya na Uganda, hatua inayolenga kuwasaidia wafugaji wadogo kupata ng’ombe bora kwa mkopo wenye masharti nafuu.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...