KILIO cha muda mrefu cha wananchi wa Kata ya Njiapanda, wilayani Moshi, kuhusu ubovu wa barabara uliosababishwa na mvua, kimeanza kupatiwa ufumbuzi baada ya Diwani wa kata hiyo kwa kushirikiana na wananchi kumwaga vifusi ili kurejesha mawasiliano ya barabara.

Hatua hiyo imewaibua Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wakidai kuendelea kutafuta fedha kwa matengenezo ya kudumu.

 Wananchi wa maeneo ya Njiapanda Mashariki, Magharibi, Samunge,  na vitongoji jirani wamekuwa wakikumbwa na changamoto kubwa ya mawasiliano  kutokana na barabara kuharibika vibaya kufuatia mafuriko ya mvua, hali inayosababisha mkwamo wa shughuli za kijamii na kiuchumi.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa wachimbaji katika eneo la mgodi wa Samunge, Samson Laizer, alisema barabara ya kuelekea migodini imeathirika kwa kiasi kikubwa na kusababisha shughuli za uchimbaji kusuasua.

Aliongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikiathiri pia wanafunzi kushindwa kwenda shule pamoja na wafanyabiashara kushindwa kusafirisha bidhaa kama kokoto, mawe, udongo na mchanga kutoka migodini.

Kwa upande wake, Faustin Abel mkazi wa Njiapanda Mashariki alisema kipindi cha mvua watoto hushindwa kwenda shule na hata wananchi wengine kushindwa kwenda ibada kutokana na ubovu wa barabara.

“Kwa kushirikiana na diwani wetu, tumeanza kuchukua hatua za dharura kwa kumwaga vifusi na kuchimba mitaro kwa nguvu za wananchi ili kurahisisha upitishaji wa magari na watu, kwa muda wakati tukisubiri matengenezo ya kudumu,” alisema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Njiapanda Mashariki, Sadick Kanyika, alisema kitongoji hicho chenye wakazi zaidi ya 7,500 kimeathirika kwa kiasi kikubwa na mafuriko, huku barabara muhimu ikiwemo ya ofisi ya mtendaji ikiharibika vibaya.

Naye Donsia Andrea mkazi wa Otomoro alisema hali hiyo imekuwa hatari zaidi kwa kina mama wajawazito na wagonjwa, akieleza kuwa baadhi yao hulazimika kujifungulia njiani kutokana na kushindwa kufikishwa hospitalini kwa wakati.

Kutokana na hali hiyo, Diwani wa Kata ya Njiapanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, John Meela, alisema wameanza hatua za dharura za kurekebisha barabara hizo kwa kushirikiana na wananchi.

“Tumeanza kuboresha barabara zilizoathiriwa na mvua kwa kumwaga vifusi kwenye maeneo korofi, zikiwemo barabara ya Samunge, Ofisi ya Kata–Otomoro, Kilototoni–Zahanati na nyinginezo. Barabara ya Samunge–Migodini ni muhimu kiuchumi kwa kuwa inahudumia shughuli za uchimbaji, hivyo inahitaji pia uwekaji wa makalvati ili kudhibiti maji ya mvua,” alisema Meela.

Alieleza kuwa tayari wamewasiliana na TARURA ambao wamefanya ukaguzi wa barabara hizo na kuahidi kutafuta fedha za dharura kwa ajili ya matengenezo ya haraka.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Moshi, Godfrey Mbena, alisema mtandao wa barabara unaohudumiwa na wakala huo katika Halmashauri ya Moshi, una urefu wa kilometa 827.71, ambapo kilometa 41.65 ni za lami, kilometa 337.16 ni za changarawe na kilometa 448.9 ni za udongo.

Alisema mvua zimeathiri kwa kiasi kikubwa barabara nyingi vijijini, ikiwemo katika kata ya Njiapanda huku changamoto kubwa ikiwa ni upungufu wa fedha kulinganisha na mahitaji halisi.

“Tumefanya tathmini ya barabara zilizoathirika na kuziwasilisha kwa ajili ya kupata fedha za matengenezo. Kwa sasa tumeomba zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya Wilaya ya  Moshi na tunaamini serikali itatoa fedha hizo ili kuanza matengenezo,” alisema.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...