Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema hana mpango wa kugombea cheo chochote cha uongozi na kwamba yuko tayari kuzungumza ukweli popote pale bila kuogopa, akisisitiza umuhimu wa uadilifu na uwajibikaji katika jamii.

Makonda ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili, mkakati unaolenga kurejesha na kuimarisha misingi ya maadili katika jamii ya Watanzania, hususan kwa vijana.

Akizungumza mbele ya wadau mbalimbali, Makonda amewataka wanahabari kubadili namna ya uandishi wa habari, akisema kwa sasa baadhi ya vyombo vya habari vimejikita zaidi katika kuripoti matukio yenye mwelekeo wa kushtua na kuvutia hisia, badala ya kuangazia habari zenye kujenga taifa.

Amesema matukio kama vifo, ufumaniaji na migogoro ya kijamii yamekuwa yakipewa nafasi kubwa zaidi kwenye mitandao na vyombo vya habari, hali ambayo kwa mujibu wake inaweza kuchangia mmomonyoko wa maadili kwa jamii.

“Kwa nini hamuelezi mazuri yanayofanywa na nchi hii? Chagueni habari zenye maadili ya Watanzania,” amesema Makonda, akisisitiza kuwa uandishi wa habari unapaswa kuwa na uwiano unaojenga na si kubomoa jamii.

Aidha, ameeleza kuwa hata baadhi ya viongozi wa dini wameanza kujihusisha zaidi na kutafuta matukio yanayovutia mitandaoni badala ya kuzingatia jukumu lao la msingi la kuhubiri maadili na kuelimisha jamii, hasa watoto na vijana.

Amesema ni muhimu kwa viongozi hao kurejea kwenye msingi wa malezi ya kiroho na kijamii kwa kujikita zaidi katika shughuli za mafunzo ya maadili mashuleni, kwenye taasisi za dini na katika jamii kwa ujumla.

Makonda pia amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nguvu kubwa ya kuathiri fikra na mienendo ya jamii, hivyo vinapaswa kuitumia nafasi hiyo kwa busara ili kuhamasisha maadili mema, uzalendo na mshikamano wa kitaifa.

Ameongeza kuwa mkakati huo wa taifa utahusisha wadau mbalimbali wakiwemo serikali, taasisi za dini, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha maadili yanarejea na kudumishwa.

Uzinduzi wa mkakati huo umeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto za kijamii zinazoongezeka, zikiwemo mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kupungua kwa malezi ya kijamii.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...