Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma


Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha shule zote za msingi na sekondari nchini zinakuwa jumuishi, ili kutoa fursa sawa za elimu kwa wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Ndugange, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Aisha Msantu Mduyah, aliyekuwa akitaka kufahamu mikakati ya serikali katika kuboresha miundombinu wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Dkt. Ndugange amesema kuwa hatua hiyo inatekelezwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Utekelezaji wa Mkakati wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2022–2026 pamoja na Waraka Namba 3 wa mwaka 2025, unaolenga kuimarisha mfumo wa kitaifa wa kuzifanya shule kuwa jumuishi.

Ameeleza kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kuendeleza vipaji vyao. Mikakati hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu rafiki kwa wanafunzi hao, ikiwemo madarasa, vyoo na njia za kupita zinazokidhi mahitaji yao.

Aidha, serikali inaendelea kuhakikisha bajeti zake zinatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa wezeshi na visaidizi, vinavyosaidia ujifunzaji kwa wanafunzi wenye changamoto mbalimbali. Vifaa hivyo vinajumuisha zana za kufundishia na kujifunzia zinazowezesha ushiriki kamili darasani.

Katika kuimarisha rasilimali watu, serikali pia inaendelea kuajiri walimu wenye utaalamu wa elimu maalum pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu waliopo ili kuwajengea uwezo wa kushughulikia wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa ufanisi zaidi.

Akitoa takwimu za hali ya sasa, Dkt. Ndugange amesema kuwa kuna shule maalum 44 za msingi na shule moja ya sekondari, sambamba na vitengo maalum 815 katika shule za awali na msingi. Pia kuna jumla ya shule jumuishi 20,889 za msingi na 6,488 za sekondari kote nchini.

Kwa upande wa wanafunzi wenye changamoto kubwa zaidi, serikali imeanzisha shule jumuishi za sekondari za bweni 53 za kitaifa pamoja na shule 3 za kutwa, ambazo zinapokea wanafunzi hao kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha miundombinu na huduma katika shule zote ili kuhakikisha zinakuwa jumuishi zaidi, na kwamba hakuna mwanafunzi atakayebaki nyuma katika kupata elimu bora kutokana na changamoto alizonazo.

Hatua hizi zinaonyesha dhamira ya serikali ya kujenga mfumo wa elimu unaozingatia usawa, ujumuishi na fursa kwa wote, huku ikiwapa wanafunzi wenye mahitaji maalum nafasi ya kufikia ndoto zao kulingana na uwezo na vipaji vyao.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...