Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema mradi wa ujenzi wa Maabara za Sayansi na Skuli ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ni muhimu kwa kuwa unaolenga kuweka misingi imara ya maendeleo ya Teknolojia, Ujuzi, na Uchumi katika jamii.

 Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Maabara za Sayansi na Skuli ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ikiwa ni shamrashamra za Miaka 62 ya Muungano.

 Amesema mradi huo utaleta manufaa makubwa kwa nchi, ikiwa ni pamoja na kutengeneza fursa za ajira, kuongeza uelewa katika sayansi na teknolojia, kushajihisha uchumi wa buluu na kuongeza tija katika kilimo.

 Aidha, Makamu wa Rais amesema elimu ni kipaumbele cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa ndiyo inayowezesha uendelezaji wa rasilimaliwatu ili kuchangia kikamilifu katika kujenga Taifa na kuleta maendeleo kwa ujumla. 

Ameongeza kwamba uwekaji wa Jiwe la Msingi unaangazia mafanikio ya Muungano wa Tanzania katika miaka 62 iliyopita, ambapo umewezesha kushirikiana zaidi, kuimarisha amani, na kustawisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika pande zote mbili za Muungano.

 Makamu wa Rais ametoa wito kwa Mshauri Elekezi na Mkandarasi wa mradi huo, kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi na kuhakikisha unafikia malengo yaliyokusudiwa. Amesema ni matarajio kuona mradi unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya hali ya juu, weledi, thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati.

Vilevile ametoa rai kwa uongozi wa SUZA kusimamia rasilimali hizo kwa uadilifu na uwazi ili kuhakikisha kuwa miundombinu inayojengwa inawezesha kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwemo kuchochea tafiti na bunifu zinazolenga kutatua changamoto halisi za jamii, hususan katika sekta za kilimo, teknolojia, utalii na mazingira. 

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Prof. Abdi Talib Abdalla amesema Jengo la Maabara ya Sayansi litakuwa kitovu muhimu katika ufundishaji wa sayansi tafiti za kisasa, bunifu na teknolojia ndani ya chuo na nchi kwa ujumla

 Amesema kupitia maabara hizo za kisasa wanafunzi na watafiti watapata mazingira bora ya kufanya majaribio tafiti shirikishi na bunifu zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali za kijamii kiuchumi na kimazingira. 

Aidha uwekezaji huo utaongeza ubora wa elimu ya sayansi na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa vitendo na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kitaifa na kimataifa.

 Pia amesema Maabara na Skuli ya Kilimo itaimarisha uwezo wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar katika kutoa huduma za ushauri elekezi, mafunzo maalum na tafiiti zinazolenga kutatua changamoto za jamii na kuchochea uchumi wa Taifa.

Mradi Maabara na Skuli ya Kilimo wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar umefadhiliwa na mradi wa Benki ya Dunia wa HEET (The Higher Education for Economic Transformation - HEET), ambapo unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 32.155.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...