Na. Jacob Kasiri - Moshi.
“Dhamira ya kuurejesha Mlima Kilimanjaro katika usafi wake wa asili imejadiliwa leo Aprili 15, 2026 mjini Moshi katika kikao cha pamoja kilichowahusisha wawakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, TANAPA na wamiliki wa Kampuni za utalii.
Uzalishaji wa taka ngumu na laini mlimani na baadae kuzishusha katika malango ya kushukia watalii imeonekana kama ndoto. Lakini ndoto hii itakuwa na matokeo chanya endapo, wenye makampuni ya utalii, waongoza wageni, Watalii na Wapagazi (wagumu) wataungana kwa pamoja kukusanya na kushusha ili kulinda mazingira na mandhari ya mlima huu unaoingiza takribani watalii elfu 65 kwa mwaka.
Akiongea namna ya kudhibiti uchafu, Mwenyekiti wa kikao hicho Bw. Michael Kilawila Mmiliki wa Kampuni ya “Coming to Africa” alisema;
“Sisi wenye Makampuni ndio tunaozalisha uchafu mlimani, hivyo ni jukumu letu kwa kushirikiana na mamlaka (KINAPA) kushusha taka hizo kwa kuwa mlima huo ni ofisi yetu. Hivyo sio vizuri kuichafua ofisi inayotuingizia kipato.”
Aidha, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro - Kamishna Msaidizi Mwandamizi Angela Nyaki alisema kuwa jitihada mbalimbali za serikali kudhibiti uchafu mlimani zinaendelea kila siku lakini bado uchafu unazalishwa mwingine.
“Ni wajibu wetu kuungana kuhakikisha uchafu tuonazalisha, tushuke nao ili kuufanya mlima wetu uwe safi, pia kumbukeni Mlima Kilimanjaro ni chanzo cha maji yanayotumika katika mji wa Moshi. Hivyo tunapochafua mlima tutambue madhara makubwa wanayapata wananchi wetu wanaotumia maji hayo.”
Sanjari na hilo pia Kamishna Nyaki aliwaomba wenye makampuni ya utalii wanapounadi mlima Kilimanjaro wauze vilele vitatu ambavyo ni Kibo, Shira na Mawenzi tofauti na sasa hivi wanauza kilele cha Kibo tu chenye urefu wa mita 5895 kutoka usawa wa bahari.
Naye, Simbo Natai - Mkurugenzi wa Kampuni ya “African Scenic” alisema; “Suala la uchafu tusiruhusu kuwa janga kwa sehemu tunayojipatia riziki, hivyo katika kikao hiki nashauri kabla ya kuanza kwa msimu wa utalii mwanzoni mwa mwezi mei, 2026 twende mlimani tukakusanye taka hizo na kuzishusha.”
David Mshana Mkurugenzi wa Kampuni ya “Enjoy Kili Ltd”, alishauri kuwa waongoza watalii(Guides) wapya kabla hawajapewa leseni ya kuongoza watalii wapandishwe mlimani kukusanya taka na kushuka nazo ili anapoongoza wageni pamoja na wapagazi awe ni mlinzi wa timu yake kuhakikisha hawatupi uchafu na kuharibu mazingira.
Mbali na mada ya taka mlimani pia agenda kama uokoaji wa wageni mlimani, waongoza watali na wapagazi kuwa na Kanzi Data na mapendekezo ya utoaji vyeti kwa watalii waliofika kileleni kwa njia ya kielektroniki zilijadiliwa na kupewa kipaumbele.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...