
-Ataka watanzania waache tabia ya kujidogosha.
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameandika historia ambayo kwa namna yoyote haiwezi kufutika kutokana na magaeuzi makubwa aliyoyafanya.
Amesema historia hiyo inaandikwa kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa, uandishi wa dira mpya ya Taifa ya 2025, kubadilisha mfumo wa elimu, kujenga madarasa mengi na shule za elimu ya amali, kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote, kupandisha bajeti ya kilimo na kuongeza upatikanaji wa huduma za umeme na maji kwa wananchi vijijini.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo jioni (Jumatano, Aprili 15, 2026) Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2026/2027.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia katika historia ya viongozi wachache wa Taifa letu waliopata heshima na bahati ya kuandika Dira ya Taifa 2050 pamoja na nyaraka nyingine muhimu za utekelezaji wa dira ikiwemo mpango wa maendeleao wa muda mrefu.”
Akielezea mafanikio kwenye sekta ya kilimo, Waziri Mkuu amesema: “Ili kuwezesha mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya kilimo mara tano kutoka shilingi bilioni 270 mwaka 2020/2021 hadi shilingi trillioni 1.23 mwaka 2025/2026. Tumeshuhudia upatikanaji wa pembejeo za kilimo na ongezeko la matumizi ya mbolea.”
Kuhusu nishati, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia katika rekodi kwa utekelezaji mkubwa wa mradi wa bwawa la umeme ambapo kwa sasa nchini kuna ziada ya umeme. “Alipokea huu mradi ukiwa katika asilimia 27 kwenda 30 ya utekelezaji. Amekamilisha mradi huo na sasa tuna ziada ya megawati zaidi ya 2,000. Tanzania ni nchi ambayo sasa ina ziada ya umeme.”
Amesema Mheshimiwa ametoa zaidi ya trilioni 1.2 za kujenga Mradi wa Gridi Imara ili kuondoa tatizo la kukatikatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kuwa Tanzania imesifiwa kwa weledi katika utafutaji wa rasilmali kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa. “Juzi imetolewa tuzo kwa kwa nchi yetu ya kufanya vizuri katika kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Tanzania ni nchi ya mfano kwenye kutafuta rasilimali kwenye kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.”
Waziri Mkuu amesema kutokana na hayo, katika mradi wa kimkakati wa reli ya kisasa tayari kipande cha tatu na cha nne kimepata fedha za kuanza ujenzi. “Vilevile, kipande cha tano nacho tayari kimepata fedha na utekelezaji wake unategemea certificates za mtekelezaji kadiri anavyokamilisha.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Watanzania waache kujidogosha kwani Tanzania imepiga hatua kubwa za kimaendeleo ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.
“Hapa Tanzania tunapenda kujidogosha hasa tusipojilinganisha na nchi nyingine. Tuache kujidogosha. Kwenye suala la umeme, hapa Afrika kuna nchi wameunganisha mikoa na mikoa tu lakini sisi kila kijiji umeme umeshafika. Na kwenye vitongoji 68,000, nusu yake umeme umeshafika na vitongoji zaidi ya 9,000 mikataba imeshasainiwa. Kwingine huko, ni mtu na solar yake au jenereta lake. Tunapaswa tujivunie kuwa tuko kwenye nchi ambayo viongozi wake maisha ya kila mtu na kuhakikisha keki ya Taifa inamfikia kila mtu,” ameongeza.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Bunge limeidhinisha sh. trilioni 12.5 ambapo kati ya fedha hizo, sh. trilioni 8.73 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. trilioni 3.76 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Vilevile, Bunge limeidhinisha sh. bilioni 225 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya fedha hizo, sh. bilioni 207.99 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. bilioni 17.02 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...