Na Mwandishi Wetu

SEKTA ya bima nchini Tanzania imeanzisha mpango mpya wa tuzo za kitaifa unaolenga kukuza ubora, ubunifu na uwajibikaji, hatua inayotarajiwa kuimarisha imani ya umma na kusaidia ukuaji endelevu.

Mpango huo, unaojulikana kama Tuzo za ATI Bima, umezinduliwa na Chama cha Wabima Tanzania (ATI), ukileta pamoja wadau wakuu katika mnyororo wa thamani wa bima, wakiwemo makampuni ya bima, madalali, mawakala na watoa huduma wa bancassurance.

Viongozi wa sekta hiyo wanasema tuzo hizo zinakuja wakati ambapo sekta inaendelea kubadilika kwa kasi, ikichochewa na maboresho ya kanuni, upanuzi wa njia za usambazaji na matumizi yanayoongezeka ya teknolojia za kidijitali ili kupanua upatikanaji wa huduma za bima.

Akizungumza leo, Mwenyekiti wa ATI, Dkt. Flora Minja, amesema  tuzo hizo zimebuniwa si tu kutambua waliofanya vizuri, bali pia kuinua viwango katika sekta nzima.

“Tuzo hizi zinaakisi dhamira ya pamoja ya sekta katika kufikia ubora na weledi,” amesema na kubainisha kuwa kutambua utendaji bora na uongozi kutachochea utekelezaji wa mbinu bora na ubunifu.

Mpango huo utahusisha makundi mbalimbali, yakiwemo Bima Bora ya Mwaka, Bima ya Maisha na Isiyo ya Maisha, pamoja na tuzo kwa madalali, mawakala, makampuni ya urejeshaji bima (reinsurance) na watoa huduma wa bancassurance.

Ameongeza kuwa pia kutakuwa na tuzo binafsi kama Mtendaji Mkuu wa Bima wa Mwaka, Kiongozi Anayechipukia na Tuzo ya Mafanikio ya Maisha.

Makundi mengine yataangazia ukuaji na ubunifu, yakitambua kampuni zinazoonesha kupanuka kwa kasi au matumizi bora ya teknolojia kuboresha huduma.

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA), Zakaria Muyengi, amesema asilimia 10 ya mapato yatakayopatikana katika hafla hiyo yatatolewa kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo.

“Tunaungana na wadau wetu katika tuzo hizi ambazo zinalenga kufungua fursa zaidi za uelewa wa bima na kujenga imani kwa watumiaji. Tutashiriki kikamilifu,” amesema.

Sekta ya bima nchini imekuwa ikionesha ukuaji wa taratibu katika miaka ya hivi karibuni, ikichochewa na mageuzi ya sera pamoja na jitihada za kuongeza matumizi ya bima kwa watu binafsi na biashara.

Wadau wanaamini kuwa kuanzishwa kwa jukwaa la kitaifa la utambuzi kutachochea zaidi maendeleo hayo kwa kuhamasisha ushindani, uwazi na utoaji bora wa huduma.

Bw. Muyengi alisema mchakato wa tuzo hizo utaongozwa na mfumo huru wa tathmini, ambapo uteuzi wa washiriki utafanyika kwa kuzingatia viashiria maalum vya utendaji ili kuhakikisha uaminifu na usawa.

Mbali na kutambua ubora, mpango huo pia unatarajiwa kuwa jukwaa la majadiliano kati ya wabima, wasimamizi na wadau wengine, hivyo kuimarisha ushirikiano na kubadilishana maarifa ndani ya sekta.

Mchakato huo utakamilika kwa hafla ya kilele itakayowakutanisha watunga sera na viongozi wa sekta kusherehekea mafanikio na kujadili mwelekeo wa baadaye wa sekta ya bima nchini .



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...