Na Janeth Raphael

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema kuwa mpango wa mkopo wa shilingi bilioni 20 uliotengwa kwa ajili ya kuwawezesha watengenezaji wa maudhui mitandaoni (content creators) umeonyesha mwitikio mkubwa kuliko ilivyotarajiwa, hali inayoashiria ongezeko kubwa la vijana wanaojihusisha na sekta ya ubunifu wa kidigitali nchini.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya 74 ya Miss World 2027, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema lengo la mkopo huo ni kuwawezesha vijana wenye vipaji lakini wenye changamoto za kifedha ili waweze kukuza ubunifu wao na kujiajiri kupitia maudhui ya kidigitali.

Makonda amesema mpango huo ulipangwa kwa nia ya kuwasaidia vijana wanaoanza safari yao ya ubunifu, hasa wale wanaokosa vifaa muhimu kama kamera bora, vifaa vya uhariri, na rasilimali nyingine za msingi zinazohitajika katika uzalishaji wa maudhui ya kisasa.

Hata hivyo, amesema tathmini ya awali imeonesha kuwa maombi yamezidi kiwango kilichotarajiwa, jambo linaloonesha wazi kuwa sekta ya content creation imekuwa na mvuto mkubwa na inakua kwa kasi nchini Tanzania.

“Hatuwezi kuchukua mkopo huu tukawapa watu ambao tayari wana uwezo mkubwa, kama kumiliki magari ya gharama kubwa au kuwa na vifaa vya kisasa. Dhamira yetu ni kumsaidia kijana wa kawaida aliye mtaani, mwenye ndoto lakini hana uwezo wa kuanza,” amesema Makonda.

Kutokana na hali hiyo, Waziri huyo amesema serikali imeamua kuahirisha kwa muda utekelezaji wa mpango huo ili kufanya maboresho muhimu, yakiwemo marekebisho ya vigezo na masharti ya mkopo huo ili kuhakikisha unawafikia walengwa sahihi.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yatalenga pia kuweka riba nafuu na masharti rahisi zaidi ili kuhakikisha mkopo huo hauwi mzigo kwa vijana, bali unakuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta ya ubunifu na ajira nchini.

Serikali imesisitiza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha vijana wengi zaidi wananufaika na fursa zilizopo kwenye uchumi wa kidigitali, ambao kwa sasa unaendelea kukua kwa kasi na kutoa nafasi kubwa za ajira na ubunifu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...