Na Janeth Raphael MichuziTv
Tanzania imeingia katika historia mpya ya sekta ya afya duniani baada ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS), mkutano ambao kwa mara ya kwanza umefanyika barani Afrika.
Mkutano huo mkubwa wa kimataifa umefunguliwa rasmi leo jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere na kuhudhuriwa na madaktari bingwa, wataalamu wa afya, viongozi wa serikali na wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania imepokea heshima kubwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa tukio hilo muhimu, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha wazi kuongezeka kwa mchango wa Afrika katika maendeleo ya huduma za afya za kibingwa duniani.
Rais Samia alisema uwepo wa wataalamu hao nchini si tu ishara ya mafanikio ya kisayansi, bali pia ni uthibitisho wa kuimarika kwa ushirikiano kati ya Afrika na dunia katika kukabiliana na magonjwa ya ubongo na mishipa ya fahamu ambayo ni miongoni mwa changamoto kubwa za kitabibu duniani.
Amesema mkutano huo unatoa nafasi muhimu kwa madaktari kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu za kisasa za matibabu, huku ukilenga kuboresha huduma kwa wagonjwa wanaokabiliwa na magonjwa ya mfumo wa fahamu katika nchi mbalimbali.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia amewashukuru madaktari bingwa kutoka mataifa mbalimbali walioshiriki kufanya upasuaji kwa wagonjwa wenye uhitaji mkubwa nchini Tanzania, akisema juhudi hizo zimeleta matumaini mapya kwa familia nyingi ambazo zilikuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa za kiafya kwa muda mrefu.
Aidha, amesema ushirikiano huo wa kitabibu ni muhimu katika kuinua kiwango cha huduma za afya nchini na kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya mtandao mpana wa kimataifa wa tiba za kibingwa.
Wakati huo huo, Rais Samia amewakaribisha washiriki wa mkutano huo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, akivitaja Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa wa vivutio vya asili, historia na utamaduni vinavyovutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Mkutano huo unatarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa ukiwa na mijadala ya kisayansi, mawasilisho ya tafiti na mafunzo mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, hatua ambayo inatarajiwa kuacha alama kubwa katika sekta ya afya barani Afrika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea Mabanda ya maonesho ya wadau wa Sekta ya Afya kabla ya kufungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...