Na Janeth Raphael - MichuziTv

Tanzania imeweka historia mpya katika sekta ya afya baada ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, mkutano ambao ni wa pili kufanyika duniani na wa kwanza barani Afrika.

Akifungua mkutano huo jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alisema hatua hiyo inaonesha heshima kubwa kwa nchi na pia kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika huduma za afya za kibobezi.

Alibainisha kuwa mkutano huo unafuata ule wa kwanza uliofanyika Februari 2024 huko Peshawar, Pakistan, akisisitiza kuwa kufanyika kwake Afrika kwa mara ya kwanza ni hatua muhimu kwa bara hilo na kwa Tanzania kama mwenyeji.

Rais Samia alieleza kuwa upasuaji wa neva ni mojawapo ya fani nyeti na ngumu zaidi katika tiba, inayohusisha kuokoa maisha na kurejesha matumaini kwa wagonjwa wenye majeraha ya ubongo, uvimbe na matatizo ya uti wa mgongo. Alisisitiza kuwa magonjwa hayo yanahitaji utaalamu wa juu, umakini na kujitolea kwa wataalamu wa afya.

Aidha, alieleza kuwa serikali inatambua umuhimu wa sekta ya afya katika maendeleo ya taifa, na inaendelea kuwekeza katika huduma za kibobezi ili kuboresha ustawi wa wananchi. Alisema taifa lenye afya bora ni msingi wa ukuaji wa uchumi, uzalishaji na utulivu wa kijamii.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za upasuaji wa neva. Idadi ya hospitali zinazotoa huduma hizo imeongezeka kutoka 2 mwaka 2020 hadi 7 kufikia Aprili 2026, hatua inayoonesha maboresho makubwa ya miundombinu na rasilimali watu.

Vilevile, idadi ya madaktari imeongezeka, ambapo madaktari wa upasuaji kwa ujumla wameongezeka kutoka 1,038 mwaka 2020 hadi 1,518 mwaka 2026. Madaktari wa upasuaji wa neva nao wameongezeka kutoka 12 hadi 37, ambapo 7 kati yao ni wanawake, hali inayoonesha kuimarika kwa ushirikishwaji wa kijinsia katika fani hiyo.

Katika upande wa teknolojia, serikali imeongeza uwekezaji katika vifaa tiba ambapo mashine za MRI zimeongezeka kutoka 7 hadi 14, CT scan kutoka 12 hadi 97, na X-ray za kidijitali kutoka 147 hadi 457, hatua inayolenga kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za uchunguzi.

Serikali pia imeeleza kuendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia mafunzo ya wataalamu, uboreshaji wa miundombinu na teknolojia, upanuzi wa huduma za telemedicine, utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali pamoja na uboreshaji wa mifumo ya kidijitali ya afya kama GOTHOMIS.

Mkutano huo unaendelea kujadili maendeleo na mustakabali wa huduma za upasuaji wa neva duniani, huku Tanzania ikitumia fursa hiyo kuonesha mafanikio yake na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...