Serikali itahakikisha vipaumbele vya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) vinaakisi uhalisia wa mchango wa Sekta Binafsi, inayotarajiwa kuchangia takribani 70% ya Pato la Taifa (GDP) ifikapo mwaka 2050.
Hatua hiyo imebainishwa na Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dr. Blandina Kilama leo Aprili 13, 2026, wakati akifungua Warsha mahususi inayolenga kutoa fursa ya kujadili kwa kina, kukusanya maoni, uzoefu na mapendekezo ya wadau kutoka Sekta ya Umma, na Sekta Binafsi kuhusu maeneo sita (6) ya kipaumbele ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano, sambamba na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“majadiliano haya yanalenga kuhakikisha kuwa mchango wa Sekta Binafsi unatambuliwa, unathaminiwa na kuingizwa kikamilifu katika uundaji na utekelezaji wa vipaumbele pamoja na mikakati ya maendeleo, ili kuimarisha ufanisi, kuongeza kasi ya utekelezaji wa FYDP IV, na kufikia matokeo yenye tija na endelevu kwa taifa” Amesema Dkt. Kilama.
Aidha, katika Warsha hiyo, washiriki watajadili mada mahususi zilizomo katika FYDP IV, ikiwemo Kujenga Uwezo wa Watu na Maendeleo ya Jamii, Kutumia Vichocheo vya Maendeleo, Mageuzi ya Sekta muhimu, Uadilifu wa Mazingira na Uhimilivu wa Tabianchi, Uchumi Imara, Jumuishi na Shindani na Kuimarisha Misingi ya Uendelevu wa Taifa.
Dkt. Kilama amesisitiza kuwa, matokeo ya warsha hiyo hayatabaki kuwa nadharia pekee, bali yatatumika katika kuboresha sera, mipango na mikakati ya maendeleo ya taifa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...